
Takwimu hizo pia zinaonesha athari kubwa kwa familia, ambapo takribani watu 340,000 wameathirika moja kwa moja.
Licha ya kupungua kwa idadi ya wahamiaji wanaowasili katika baadhi ya maeneo, shirika hilo linaonya kuwa njia za uhamiaji si salama bali zinazidi kuwa hatari.
Njia zinabadilika, hatari bado ipo
Matokeo hayo, yaliyotokana na mifumo ya ufuatiliaji ya IOM, yanaonesha kuwa mienendo ya uhamiaji duniani inabadilika kutokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na sera kali za mipaka.
“Njia za uhamiaji zinabadilika kutokana na migogoro, shinikizo la tabianchi na mabadiliko ya sera, lakini hatari bado ni kubwa,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope.
Ameongeza kuwa “Nyuma ya takwimu hizi kuna watu wanaochukua safari hatari na familia zinazobaki zikisubiri taarifa ambazo huenda zisipatikane kamwe.”
Kupungua kwa wanaowasili hakumaanishi usalama
Ripoti inaeleza kuwa kupungua kwa idadi ya wahamiaji wanaowasili katika maeneo kama Ulaya na Amerika hakumaanishi shinikizo la uhamiaji limepungua. Badala yake, wahamiaji wanachukua njia mbadala ambazo mara nyingi ni hatari zaidi.
Kwa mujibu wa takwimu za ripoti hiyo katika bara la Amerika, safari za kuelekea kaskazini kupitia Amerika ya Kati zilipungua kwa kiasi kikubwa, huku Ulaya ikishuhudia mabadiliko ya aina ya wahamiaji wanaowasili, ambapo raia wa Bangladesh walikuwa kundi kubwa zaidi.
Njia za Afrika zinazidi kuwa tata
Barani Afrika, IOM inasema mienendo ya uhamiaji inaendelea kubadilika. Safari kutoka Pembe ya Afrika kuelekea Saudi Arabia zilipungua kidogo lakini bado ziko juu ikilinganishwa na mwaka 2023.
Wakati huo huo, safari kutoka Afrika Mashariki kuelekea kusini mwa bara hilo ziliongezeka, zikichochewa na mahitaji ya ajira.
Katika njia ya bahari ya Atlantiki kutoka Afrika Magharibi kuelekea Visiwa vya Canary, idadi ya wanaowasili ilipungua, lakini safari zimekuwa ndefu zaidi na hatari zaidi.
Maelfu wamekwama katika mazingira magumu
Takwimu za IOM pia zinaonesha maelfu ya wahamiaji wamekwama katika maeneo ya mipakani bila huduma muhimu kama makazi, huduma za afya na ulinzi.
Kuongezeka kwa urejeshwaji wa wahamiaji na uhamishaji pia kunaweka mzigo mkubwa kwa huduma za jamii.
“Kubadilika kwa njia hakumaanishi kupungua kwa madhara,” shirika hilo limesisitiza, likionya kuwa safari zinazozidi kuwa hatarishi zinaongeza vifo na mateso kwa familia zilizoachwa nyuma.
Wito wa hatua za haraka kimataifa
Kabla ya Mkutano wa Kimataifa wa Mapitio ya Uhamiaji mwezi Mei, IOM inatoa wito kwa nchi kuongeza juhudi za kulinda wahamiaji na kuzuia vifo.
“Kuokoa maisha kunahitaji ushirikiano mkubwa wa kimataifa na uwekezaji endelevu katika suluhisho zinazotegemea ushahidi,” shirika hilo linasema.
Ujumbe wake ni wazi, kupungua kwa idadi ya wanaosafiri hakumaanishi safari ni salama zaidi na bila hatua za pamoja, gharama ya kibinadamu itaendelea kuongezeka.