Hali ya sintofahamu inaendelea kuzunguka uwezekano wa mazungumzo kati ya Marekani na Iran nchini Pakistan, huku kukiwa bado hakuna uthibitisho kama yatafanyika.
Kufungwa kwa mlangobahari wa Hormuz kunaathiri biashara kwa kiwango cha kimataifa.
Wakati huo huo, mvutano unaendelea katika Mlango Bahari wa Hormuz, ukizua hofu kuhusu usalama wa usafiri wa majini, wakati mgogoro wa kibinadamu nchini Lebanon ukiendelea licha ya sitisho la mapigano.
Mgogoro wachochea mshtuko wa nishati duniani
Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umechochea kile kinachotajwa kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa nishati katika kizazi hiki, ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres.
Akihutubia kwa njia ya video katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi Petersberg Climate Dialogue, alisema “Unafanya ukweli mmoja kuwa wazi kabisa, nishati ya mafuta ya kisukuku si tu inaharibu sayari yetu pia inashikilia uchumi mateka.”
Amesisitiza kuwa nishati safi ndiyo njia salama zaidi ya siku zijazo na kutoa wito wa kuharakisha uwekezaji, kuimarisha miundombinu na kuongeza ufadhili ili kusaidia mabadiliko ya kimataifa kuelekea nishati mbadala.
Mabaharia wakili kiamsha kinywa ndani ya meli ya usafirishaji wa baharini.
Mabaharia wamekwama katika Mlango Bahari wa Hormuz
Huku usafirishaji wa majini ukisimama karibu kabisa katika Mlango Bahari wa Hormuz, mkuu wa Shirika la Kimatafa la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Majini (IMO) ameangazia mateso ya mabaharia waliokwama baharini.
Akizungumza mjini Singapore, Katibu Mkuu wa IMO Arsenio Dominguez ameeleza hali ya msongo wa mawazo na uchovu mkubwa unaowakabili walioko melini.
Takribani mabaharia 20,000 na karibu meli 2,000 bado wamekwama katika njia hiyo muhimu ya kimataifa, ambayo kabla ya vita ilikuwa inapitia karibu robo ya biashara ya mafuta duniani pamoja na kiasi kikubwa cha gesi asilia na mbolea.
Amebainisha kuwa baadhi ya nchi zimeanzisha huduma za msaada wa simu na nyingine kutoa chakula, huku akitoa wito wa upatikanaji wa mtandao wa intaneti bure ili mabaharia waweze kuwasiliana na familia zao.
Ukuaji wa uchumi Asia-Pasifiki wapungua, mfumuko wa bei wapanda
Matarajio ya uchumi katika eneo la Asia na Pasifiki yanazidi kudhoofika kutokana na mvutano wa kimataifa unaoongeza gharama na kuvuruga biashara, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Tume ya Kiuchumi na Kijamii kwa nchi za Asia-Pasifiki (ESCAP).
Ripoti hiyo inaonesha kuwa ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea unatarajiwa kushuka hadi asilimia 4.0 mwaka 2026, kutoka asilimia 4.6 mwaka 2025, huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kupanda hadi asilimia 4.6 kutoka asilimia 3.5.
Ripoti pia inaonya kuwa makadirio haya yanakabiliwa na kutokuwa na uhakika mkubwa, huku mgogoro wa Mashariki ya Kati ukiongeza shinikizo kupitia kupanda kwa bei ya nishati na chakula pamoja na kupungua kwa mahitaji ya kimataifa.
Msichana mdogo anakula mkate nje ya makazi ya muda ya familia yake huko Gaza.
Gharama za maisha zapanda, changamoto za kifedha zazidi
Kupanda kwa mfumuko wa bei kunaongeza gharama za maisha, hasa kwa kaya zenye kipato cha chini, wakati madeni makubwa ya serikali na uwezekano wa kupanda kwa viwango vya riba vinaweza kupunguza uwezo wa serikali kuchukua hatua.
Hata hivyo, licha ya changamoto hizi, eneo hilo linatarajiwa kubaki na kasi kubwa ya ukuaji ikilinganishwa na maeneo mengine yanayoendelea, ingawa ESCAP inasisitiza kuwa kuimarisha mahitaji ya ndani na ushirikiano wa kikanda kutakuwa muhimu katika kudumisha ukuaji huo.