Nigeria. Mwanamuziki maarufu wa Nigeria na mmoja wa waliokuwa wanaunda kundi lililovunjika la P-Square, Peter Okoye maarufu ‘Mr P’, amezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutangaza kuwa anabadilisha tarehe yake ya kuzaliwa.

Kupitia ujumbe aliouchapisha jana Jumatatu, Aprili 20, 2026 kwenye akaunti yake rasmi ya X (Twitter), msanii huyo alisema amebadili tarehe ya kuzaliwa kutoka Novemba 18 kwenda Novemba 30.

“Ninapenda kuwajulisha rasmi kuwa ninabadilisha tarehe ya kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa. Kuanzia sasa, Novemba 18 haitakuwa tena siku yangu ya kusherehekea birthday. Tafadhali tambueni kwamba sitapokea ujumbe wala zawadi zozote siku hiyo.

“Kuanzia sasa, siku yangu ya kuzaliwa itakuwa inaadhimishwa Novemba 30. Huu ni uamuzi binafsi, na ninathamini sana uelewa wenu,” aliandika

Hata hivyo, hadi taarifa hii inaandikwa, Peter hakutoa maelezo zaidi kuhusu sababu zilizomfanya achukue uamuzi huo.

Msanii huyo alipata umaarufu mkubwa akiwa sehemu ya kundi la P-Square pamoja na kaka yake pacha Paul Okoye maarufu kama Rudeboy. Kundi hilo liliwahi kutikisa muziki wa Afrika katika miaka ya 2000 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2010 kupitia nyimbo nyingi zilizopendwa na mashabiki.

Wasanii waliokuwa wanaunda kundi la muziki la P-Square kutoka Nigeria ambao ni Peter Okoye maarufu Mr P na Paul Okoye marufu Rudeboy (mwenye rasta). Picha na Mtandao

Hata hivyo, migogoro ya ndani ilianza kujitokeza na hatimaye kusababisha kuvunjika kwa kundi hilo. Mgogoro wao ulianza kujulikana hadharani mwaka 2015, ukiwa unahusishwa zaidi na masuala ya usimamizi wa kazi zao yaliyokuwa yakisimamiwa na kaka yao mkubwa, Jude Okoye.

Tofauti za maoni kuhusu mgao wa mapato ya mirabaha, udhibiti wa ubunifu wa kazi zao na kile kilichodaiwa kuwa kuingiliwa kwa masuala ya familia, vilizidi kuongeza mgogoro kati yao.

Hatimaye mwaka 2017 kundi la P-Square lilivunjika rasmi, huku kila mmoja akianza safari ya muziki wa kujitegemea Peter akitumia jina la Mr P na Paul akibaki na jina la Rudeboy.

Baada ya miaka kadhaa ya kutengana, pacha hao waliamua kumaliza tofauti zao Novemba 2021. Tukio hilo lilifurahisha mashabiki wengi barani Afrika na sehemu nyingine duniani. Upatanisho wao uliambatana na kuonekana pamoja kwenye matamasha, maonyesho mbalimbali pamoja na kutoa kazi mpya, ingawa mafanikio yake hayakufikia kiwango kikubwa kama ilivyokuwa katika enzi zao za awali.

Licha ya kurejea pamoja, taarifa zinaeleza kuwa mvutano ulianza kutokea tena baadaye, ukihusisha masuala ya kifedha, usimamizi wa mirabaha pamoja na muundo wa kampuni zinazohusiana na katalogi ya muziki wao.

Baadaye Peter alidai kuwepo kwa dosari katika mfumo wa zamani wa usimamizi wa kazi zao. Jambo lililosababisha mijadala mipya na hata hatua za kisheria zilichukuliwa kwa baadhi ya wanafamilia wa familia ya Okoye. Hivyo basi pengine kutokana na yote yaliyotokea ndiyo sababu ya mwanamuziki huyo kutangaza kubadili tarehe ya siku yake ya kuzaliwa kwa lengo la kujitenga na pacha wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *