“Uongozi wa kina mama bado uko chini. Sisi ni wachache sana katika bunge, lakini tunajitahidi kusimama imara,” anasema.

Akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili Bi. Madowo amesema, licha ya Katiba ya Kenya kutoa haki sawa kwa wote kupata fursa za uongozi na haki zingine, hali halisi mashinani bado inaathiriwa na mila na mitazamo ya kijamii.

Mila na desturi zinazokwamisha haki za wanawake Siaya

Akiangazia jamii ya Wajaluo anakotoka na kuwakilisha, Madowo anasema baadhi ya mila bado zinawanyima wanawake haki za msingi, hasa katika masuala ya urithi.

“Mila zinasema mama hana haki ya kurithi mali ya baba yake, hana haki za kurithi mali ya mume wake. Hii ni changamoto kubwa na hasa kwa wajane wengi,” anafafanua.

Anaongeza kuwa wanawake wengi huachwa bila mali wala msaada baada ya vifo vya waume zao, hali inayowaweka katika mazingira magumu ya kiuchumi.

Elimu na uhamasishaji kama silaha ya mabadiliko

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Bi. Madowo amekuwa akiendesha mikutano ya uhamasishaji katika jamii.

“Tumekuwa na vikao vingi kuwaelimisha watu kwamba Katiba inatoa haki sawa kwa wanawake na wanaume,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kuwa mabadiliko ya mitazamo hayawezi kutokea mara moja,

“Huwezi kubadilisha fikra za watu kwa siku moja. Ni mchakato unaohitaji muda na uvumilivu.”

Mwanamke mmoja Mwafrika mwenye kifuniko kichwani ameketi kwenye dawati katika studio, akizungumza kwenye kipaza sauti. Nyuma yake kuna skrini za bluu zinazoonyesha ramani ya ulimwengu.

Sheria ya kulinda wajane: Hatua ya kihistoria

Katika juhudi za kuleta mabadiliko ya kisheria, Kaunti ya Siaya imepitisha sheria ya kulinda wajane hatua ambayo Madowo anaiona kama mafanikio makubwa.

“Tumepiga hatua kama kaunti ya kwanza kupitisha sheria ya kulinda wajane. Hii ni hatua muhimu sana,” anasema kwa fahari.

Sheria hiyo inalenga kuhakikisha wajane wanabaki na haki ya kuishi katika ardhi zao na kulindwa dhidi ya kunyanyaswa au kunyang’anywa mali.

Msaada wa kisheria mashinani

Changamoto nyingine kubwa ni gharama za kufikia haki kupitia mahakama. Ili kushughulikia hili, Bi. Madowo na wenzake wameanzisha mpango wa msaada wa kisheria kwa wananchi mashinani.

Kwa kushirikiana na Mahakama ya Siaya, wamepeleka huduma za kisheria karibu na wananchi kupitia kile kinachoitwa “Msaada wa Kisheria mashinani.”

Anasema “Tumewaleta mawakili wanaotoa huduma bure ili kusaidia wananchi kupata haki zao bila gharama au probono”.

Mpango huu unalenga kuwasaidia hasa wanawake na wajane ambao hawana uwezo wa kugharamia kesi mahakamani.

Ushirikiano wa serikali na matumaini ya mabadiliko

Madowo anaamini kuwa juhudi hizi zinaungwa mkono na mwelekeo wa kitaifa wa kuimarisha haki za wanawake.

Anataja uongozi wa kitaifa na taasisi za serikali kama ishara kuwa kuna nia ya kweli ya kuleta mabadiliko.

“Mahali penye nia pana njia. Tunaona mabadiliko yakija, na wanawake lazima wawe na imani,” anasema.

Ujumbe kwa wanawake: Simama na utetee haki zako

Katika hitimisho lake, Bi. Madowo anatoa wito kwa wanawake kutokaa kimya wanaponyanyaswa au kunyimwa haki.

“Tusinyamaze tunaponyanyaswa. Tujitokeze na kupigania haki zetu,” amesisitiza.

Kwa mtazamo wake, safari ya usawa wa kijinsia bado ni ndefu, lakini hatua zinazochukuliwa sasa zinaweka msingi wa mabadiliko ya kudumu katika Kaunti ya Siaya na kote nchini Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *