
Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Bongofleva, Sefu Shabani maarufu Matonya ni kati ya waimbaji waliotikisa Afrika Mashariki, albamu zake tatu kuhusu mapenzi na maisha kwa ujumla zilimpatia umaarufu na mashabiki wengi wakati huo.
Baadhi ya nyimbo zake maarufu ni Uaminifu, Vailet, Siamini, Mule Mule, Anita, Spair Tairi, Zilipendwa, Dunia Mapito, Taxi Bubu na kadhalika.
Kutoka maisha ya kawaida hadi kujenga heshima katika muziki, safari ya Matonya tangu mwanzo hadi kuja kuisimamisha chapa yake, ni matokeo ya kipaji, nia, juhudi na hata bahati pia.
Staa huyo alizaliwa katika Hospitali ya Bombo mkoani Tanga, ambapo alikulia na kusoma shule ya msingi Mkwakwani na baadaye kujiunga na shule ya sekondari Sahare. Akiwa bado mwanafunzi, Matonya aliyepewa jina hilo na marafiki, alianza kujihusisha na muziki akiwa miongoni mwa vijana watatu waliounda kundi lililojulikana kama Hard Boys Family.
Kupitia kundi hilo, walijifunza na kujijenga kwa kukutana na wasanii wakubwa wa wakati huo kama Wagosi wa Kaya na Profesa Jay, ambao walikuwa na makazi Tanga. Hii ilikuwa hatua muhimu iliyompa mwanga wa kuelekea kwenye muziki wa kibiashara, hasa ikizingatiwa kuwa Profesa Jay alikuwa akifanya kazi Tanga kipindi hicho, hivyo kuwa karibu naye kulimpa nafasi ya kujifunza kwa vitendo.
Hata hivyo, Matonya hakumaliza masomo yake ya sekondari kwani aliishia kidato cha tatu kutokana na kile alichotaja kama kuingia katika shughuli za biashara mapema.
Kwa upande mwingine, uamuzi huo ambao kwa wengine ungeonekana kama kikwazo, kwake ulikuwa mwanzo wa kujitafuta ili kufanikiwa kimuziki. Na punde tu alianza aliporekodi katika studio ya Motika Records iliyokuwa ikimilikiwa na hayati Abel Loshilaa Motika aliyekuwa maarufu Mr Ebbo, hapa ndipo alipoanza kuonja ladha ya studio na kurekodi kazi zake za mwanzo.
Hata hivyo, mafanikio makubwa yalikuja alipokutana na mtayarishaji Miikka ‘Mwamba’ Kari ambaye alisimamia utayarishaji wa wimbo wake, Uaminifu (2003) uliomtambulisha vizuri.
Wimbo huo haukuwa tu maarufu bali pia ulibeba jina la albamu yake ya kwanza, na kuanzia hapo ndipo jina la Matonya likaanza kusikika kwa nguvu katika tasnia ya muziki nchini.
Utakumbuka Miikka Mwamba, mzaliwa wa Finland ambaye alifanya kazi FM Studio kuanzia mwaka 1999 hadi 2004, amewatoa wasanii wengi akiwemo Matonya, Daz Nundaz, Banana Zorro na kadhalika. Katika kipindi hicho cha mwanzoni, kipato chake hakikuwa kikubwa sana, kwa mujibu wa Matonya fedha yake ya kwanza kubwa aliyoipata kupitia muziki ilikuwa Sh70,000.
Fedha hiyo alilipwa baada ya kutumbuiza katika uzinduzi wa albamu ya Bwana Misosi, Mabinti wa Kitanga (2003), akiwa kama msanii wa utangulizi.
Aliendelea kushiriki katika ziara (tour) ya kuitangaza albamu hiyo ya Bwana Misosi, jambo lililomfanya kujenga zaidi jina lake mbele ya mashabiki akiwa kama mwimbaji anayekuja kwa kasi.
Miaka mitatu baadaye, mambo yakabadilika kabisa kwa Matonya, hiyo ni baada ya kuachia albamu yake ya pili, Siamini (2006) ambayo ndiyo iliyomweka rasmi kwenye ramani ya Bongofleva na kumfanya kuwa miongoni mwa wasanii wakubwa wa wakati huo.
Tofauti na albamu yake ya kwanza, safari hii alifanya kazi na mtayarishaji marehemu Roy, ambaye alifanikiwa kutengeneza nyimbo zilizotikisa kama Siamini na Vailet.
Kwa mujibu wa Matonya, nyimbo hizi mbili zilirekodiwa ndani ya siku moja tu, jambo linaloonyesha namna ambavyo alikuwa na ubunifu wa kipekee studio.
Umaarufu wake uliendelea kukua baada ya kutoa wimbo ‘Dunia Mapito’ ambao uliwafanya watu wengi kuitafuta albamu yake hiyo (Siamini). Hii iliongeza mauzo ya albamu na kuthibitisha kuwa Matonya hakuwa msanii wa kubahatisha bali mwenye uwezo wa kutoa kazi zinazogusa jamii.
Baadaye, alikuja kutoa albamu yake ya tatu, Anita (2008), wimbo huo uliobeba albamu hii alimshirikisha Lady Jaydee, mwanamuziki aliyetoka na ngoma yake, Machozi (2000) chini ya MJ Records.
Aliyekuwa mume na meneja wa Lady Jaydee, hayati Gardner G. Habash ndiye alimshauri Matonya kumshirikisha Jide katika wimbo huo baada ya kuusikia kabla ya kutoka.
Ushirikiano huo uliifanya ‘Anita’ kuwa moja ya nyimbo zilizofanikiwa sana katika kazi zake nyingi alizotoa, na ndani ya muda mfupi anadai kuwa uliweza kumuingizia fedha kiasi cha Sh70 milioni.
Wimbo huo uliotayarishwa na Mandugu Digital, licha ya video yake kuchelewa kupandishwa YouTube ikiwekwa 2017, tayari imeshatazamwa zaidi ya mara milioni 11, ikiwa ndiyo kazi yake yenye mafanikio zaidi katika mtandao.
Hivyo kwa ujumla Matonya ametoa albamu hizo tatu, na kushinda jumla ya tuzo nane tano za ndani na tatu za kimataifa katika nchi za Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda. Amefanya shoo za ndani na nje ya Afrika, ikiwa ni pamoja na baadhi ya nchi za Ulaya, jambo linalothibitisha ukubwa wake.