
London. Kocha wa Chelsea Liam Rosenior ameikosoa vikali timu yake ya Chelsea baada ya kupokea kipigo cha aibu dhidi ya Brighton & Hove Albion, akisema kiwango chao “Hakikubaliki na kisicho na utetezi wowote.”
Brighton waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Chelsea, hali iliyoongeza presha kwa Rosenior huku mwenendo mbaya wa timu hiyo ukiendelea. Hii ilikuwa ni mechi ya tano mfululizo kwa Chelsea kupoteza za Premier League bila hata kufunga bao, jambo ambalo halijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 100 kwenye timu hiyo.
Matokeo hayo yamezima kwa kiasi kikubwa matumaini yao ya kufuzu kwa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) kwani sasa wapo nafasi ya saba na pointi 48 ikiwa ndiyo timu ambayo imefanya vibaya zaidi kwenye ligi hiyo katika michezo mitano iliyopita.
Akizungumza kwa hasira baada ya mechi, Rosenior hakuficha chochote, akisisitiza kuwa mabadiliko “makubwa na ya haraka” yanahitajika. Aliwataka wachezaji wake “kujiangalia kwenye kioo” na akawalaumu kwa kukosa taaluma na kujituma uwanjani.
“Kilichotokea hakikubaliki kwa kila upande wa mchezo,” alisema. “Naumia sana. Mtazamo wa wachezaji haukubaliki. Nimekuwa nikiwatetea mara kwa mara, lakini kiwango cha leo hakiwezi kutetewa.”
Aliongeza kuwa namna walivyofungwa mabao, walivyoshindwa mapambano ya ana kwa ana na kukosa nguvu ya kucheza kwa kasi ni mambo yanayohitaji kubadilika mara moja.”
Hata hivyo, alikiri kuwa yeye pia anawajibika, aliweka wazi kuwa wachezaji nao lazima wachukue lawama kwa kiwango walichoonyesha.
Rosenior pia alikosoa ukosefu wa ujasiri uliopelekea bao la kwanza la Brighton lililofungwa mapema na Ferdi Kadioglu ndani ya dakika tatu za mwanzo. Alisema kiwango cha kitaaluma hakikuwepo kabisa, na akakiri kuwa huo ulikuwa usiku mgumu zaidi kwake katika maisha yake ya ukocha.
Kuhusu swali la kama bado anaungwa mkono na wachezaji, Rosenior alisema: “Sio suala la kunichezea mimi, ni suala la kuichezea klabu na jezi yake na kucheza ili kushinda.”
Baada ya kichapo hicho, Chelsea imeshuka hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nyuma kwa alama saba dhidi ya timu iliyo nafasi ya tano. Pia mashabiki waliokuwa uwanjani walionesha hasira zao wazi kwa kumzomea kocha huyo.
Rosenior alisema anaelewa hasira za mashabiki na kusisitiza kuwa jukumu hilo liko mabegani mwake. Hata hivyo, alisisitiza kuwa atalazimika kuchagua upya kikosi cha kuaminika kabla ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Leeds United itakayochezwa Wembley.
“Chelsea inapaswa kuwakilisha mapambano, moyo na dhamira na hayo yote hayakuonekana kabisa leo,” alimaliza kusema.