
Dar es Salaam. Tume ya Uchunguzi wa matukio hayo iliyoundwa na Rais Samia na kuongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othmna Chande, imesema uchunguzi wake kilichofanyika Oktoba 29, 2025 tumebaini hayakuwa maandamano ya amani.
Akifafanua kilichotokea, Jaji Chande amesema vijana wa makundi mbalimbali wakiwemo waendesha pikipiki, waliandaliwa na kupewa mafunzo maalumu ili kushiriki vurugu hizo zilizosababisha uvunjifu wa amani na tishio la usalama nchini.
“Baada ya uchunguzi kwa kuzingatia sheria za nchi na za kikanda yaliyotokea hayakuwa maadamano, kwa sababu nne; kwanza hayakuzingatia sheria kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambayo kwa sheria za kimataifa ni kutoa taarifa,” amesema.
Ameongeza kuwa kufanya ghasia siku ya uchaguzi ilikuwa ni kupoka haki ya wananchi kushiriki uchaguzi ni kinyume cha sheria na za nchi na kimataifa, akifafanua kuwa hiyo pia ilionyesha kuwa hayo hayakuwa maandamano ya amani.
“Tatu, washiriki wa vurugu hizo walibeba silaha mbalimbali, bunduki, marungu, viberiti na manati, hii ni kinyume na sheria za maandamano ya amani za kitaifa na kimataifa ukiwemo mkataba wa Afrika,” ameongeza.
Amefichua kuwa, Tume ilibaini kuwa vurugu hizo ziliratibiwa, kupangwa na kutumia watu wasio na uelewa wa kuitosha kufika maeneo mbalimbali kuzunguka vyuoni, masokoni na maeneo mengine kuandikisha watu kuwashawishi watu kushiriki maandamano hayo.
Ameongeza kuwa wapo vijana waliowekwa pamoja na kupewa mafunzo kuwa sehemu ya kuanzisha na kushiriki vurugu hizo na kuwa walioratibu vurugu hizo hawakushiriki wala kukamatwa kwenye vurugu hizo.
“Kijana mmoja Usa River Arusha alishawishiwa alipwe Sh50,000 ili ashiriki maandamano, akiahidiwa angepewa Sh5 milioni akishiriki maandamano,” amesema Jaji Chande akitaja mbinu mbalimbali zilizotumiwa na waandamanaji hao.