
Dar es Salaam. Kadri siku zinavyosogea kuelekea uchaguzi mkuu wa Kenya wa 2027, siasa za nchi hiyo zinaingia katika hatua mpya yenye mikondo inayokinzana waziwazi, huku vigogo wakijenga ngome zao na makundi mapya yakichipuka kwa kasi.
Mvutano uliokuwa umejificha ndani ya muungano, sasa unajitokeza hadharani, ukiashiria mapambano ya wazi ya nani atachukua usukani wa taifa hilo.
Uamuzi wa vikao vya ngazi za juu vya Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kusitisha mazungumzo ya muungano na United Democratic Alliance (UDA) umefungua ukurasa mpya wa mchuano wa makundi.
Hatua hiyo si ya kawaida katika mazingira ambayo serikali ilikuwa imejengwa kwa mazungumzo kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, aliyetikisa siasa za upinzani wa taifa hilo kwa miongo kadhaa.
Wachambuzi wa siasa nchini humo wanaona kusitishwa kwa mazungumzo hayo kunatuma ujumbe mkubwa kwamba ndani ya ODM kuna sauti zinazotaka chama kijisimamie badala ya kuyeyuka ndani ya mfumo wa pamoja na Serikali ya Rais Ruto.
Ni katika mazingira hayo ndipo kundi jipya linalojizolea umaarufu la ‘Linda Mwananchi’ linajitokeza kwa nguvu, likiongozwa na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna na Gavana wa Siaya, James Orengo.
Inaelezwa kwamba kundi hilo linatoa uwezekano wa Sifuna kuwania urais mwaka 2027, hatua inayoweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa ushindani.
Ushawishi wa Linda Mwananchi
Huku likijijenga majukwaani, hasa kwa kulenga wanasiasa vijana, kundi la Linda Mwananchi tayari limeweka msimamo mkali kwa kutangaza kutomuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi ujao. Kauli hiyo inaashiria kuibuka kwa safu mpya isiyofungamana na serikali wala upinzani wa sasa.
“Mikakati yetu ni kuwa na vuguvugu imara ambalo litatikisa nchi na kusababisha Wakenya wayaone mambo kwa njia tofauti,” alisema Sifuna katika mahojiano na kituo cha redio hivi karibuni, akionyesha wazi dhamira ya kubadili mwelekeo wa mjadala wa kisiasa nchini humo.
Kwa sasa, Linda Mwananchi haionekani kuegemea upande wa upinzani unaoongozwa na Kalonzo Musyoka au aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua. Hali hiyo inalifanya kundi hilo kuwa na nguvu ya kipekee, likiwa huru kupanga mikakati yake bila kubanwa na muungano uliopo.
Katika hesabu hizo, unatajwa pia uwezekano wa tiketi ya pamoja kati ya Sifuna na Kalonzo kama moja ya mikondo inayoweza kubadili mizani ya kisiasa, hasa ikiwa utaungwa mkono na makundi yanayotafuta mabadiliko nje ya mfumo uliopo.
ODM yagawanyika
Wakati kundi la Linda Mwananchi likijijenga, ndani ya ODM mvutano unachukua sura ya mapambano ya misingi ya chama. James Orengo, mmoja wa vigogo wa chama hicho, amejitokeza hadharani kupinga mwelekeo wa ushirikiano wa chama hicho na UDA, akisisitiza kuwa chama kinapoteza falsafa yake ya uongozi.
“Sisi bado ni wanachama wa ODM, wala hatulengi kuondoka chamani. Tunapambana na kupigana ndani ya chama,” amesema hivi karibuni, akionyesha kuwa mapambano hayo ni ya ndani lakini yenye athari kubwa kwa mustakabali wa chama, akionya kuwa ushirikiano huo unaweza kudhoofisha kabisa chama hicho.
Akionesha uimara na mwelekeo wa chama hicho kuelekea uchaguzi huo ujao licha ya migawanyiko hiyo, Orengo amesema: “Chama kilianzishwa kuendeleza msingi na uongozi bora, lakini kwa sasa hilo halifanyiki. Hatuwezi kusema kuwa hatutakuwa na mgombea wa urais kwa sababu ODM ni chama ambacho kimekuwa na mwongozo imara na lazima kisalie dhabiti.”
Hoja ya kuwa na mgombea wa urais imekuwa kitovu cha mjadala huo, huku viongozi wa Linda Mwananchi wakisisitiza kuwa hatua hiyo itafungua njia mpya baada ya kifo cha Raila. Bila hilo, kuna hofu kuwa chama kinaweza kupoteza mwelekeo na hata kupungua nguvu zake bungeni.
Hata hivyo, mvutano huo unachochewa zaidi na kauli kali kutoka ndani ya chama, ambako kiongozi mkuu wa chama hicho, Oburu Oginga, amefichua kwamba kulikuwa na msuguano kati ya Raila Odinga na Sifuna kabla ya kifo chake.
“Nilichojua ni kwamba Raila Odinga hakuwa na furaha na yale ambayo Sifuna alikuwa akifanya. Sifuna alimwaibisha Kakamega, aliandaa baadhi ya vijana waliokuwa wakipiga kelele,” amesema.
Wakati haya yakiendelea, kiongozi wa UDA, Geoffrey Ruku, amesema: “Wale wanaotafuta viti watafute viti, lakini wasitafute kiti cha Rais na Naibu wa Rais,” huku Rais William Ruto akiwaonya wanaojaribu kuvuruga ushirikiano huo kuwa atawakomesha.
“Wale watu wanajaribu kuvigonganisha vyama vyetu vya UDA na ODM, mimi nitawakomesha. Hatutaki siasa za kuvipiganisha vyama vyetu, tunaweza kushinda tukiwa pamoja,” amesema Rais Ruto hivi karibuni.
Ndani ya mvutano huo unaochanganya mikakati, misimamo na hisia za kisiasa, Kenya inaingia katika kipindi ambacho siasa zake zinachorwa upya. Makundi yanajipanga, vigogo wanacharuana na kila upande unajaribu kujenga ushawishi kabla ya mapambano makubwa ya 2027.
Katika taswira hiyo, wachambuzi wa siasa nchini humo wanasema mchuano huo unaibua picha kuwa uchaguzi ujao utakuwa wa ushindani wa mikondo ya fikra, nguvu za makundi na uwezo wa wanasiasa kujenga imani kwa wapiga kura. Wanataja kuwa kadri joto linavyozidi kupanda, ndivyo nafasi ya mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini Kenya inavyozidi kuibuka huku makundi yakijijenga.
Aidha, kwa siasa za taifa hilo, hali hiyo ni ya kawaida kwa sababu kila uchaguzi unapokaribia, makundi ya kisiasa huvunjika na kuibuka ushirikiano mpya unaobadili uelekeo wa siasa na nguvu za wagombea nyakati zote za chaguzi za Kenya.