
Dar es Salaam. Baada ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 kuwasilisha ripoti yake, Chama cha ACT Wazalendo kimesema hitimisho la tume hiyo lilitarajiwa kutokana na muundo wake, wajumbe wake na hadidu rejea zake.
ACT Wazalendo imeeleza hayo baada ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mohamed Chande, kuwasilisha ripoti ya uchunguzi Aprili 23, 2026 ambapo pamoja na mambo mengine, ilieleza sababu za ghasia za Oktoba 29, vichocheo vyake na mapendekezo ya kufanyika uchunguzi zaidi.
Tume hiyo imetaja vichocheo vya ghasia hizo za Oktoba 29 kuwa ni kauli za baadhi ya wanasiasa ambazo ziligeuka kuwa kauli mbiu za baadhi ya waliokuwa wakifanya ghasia, ikiwemo “No Reforms, No Election”, “Oktoba Tunatiki”, “Oktoba Tunatoka”, “Samia Must Go”. Wengine ni waliokatwa kwenye kugombea katika ngazi ya vyama, wakaona ghasia zilizokuwa zinafanywa zingewasaidia chini kwa chini.
Kufuatia ripoti hiyo ya tume, Naibu Katibu wa Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi wa ACT Wazalendo, Mbarala Maharagande, kupitia taarifa aliyoitoa kwa waandishi wa habari leo Aprili 23, 2026, amesema:
“Chama kinasimama imara katika msimamo wake wa kukataa kile kinachoitwa Tume ya Chande, ambayo tangu mwanzo tulieleza kuwa haina uhuru na imeundwa kama chombo cha kulinda wahusika badala ya kutoa haki,” Maharagande ameeleza.
Amesema kuwa ripoti iliyowasilishwa leo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan ina hitimisho ambalo lilitarajiwa kabisa kutokana na muundo wake, wajumbe wake na hadidu rejea za tume hiyo.
“ACT Wazalendo tunaomboleza kila maisha yaliyopotezwa na kila familia iliyopata madhila kufuatia matukio ya tarehe 29 Oktoba na athari zake. Uponyaji wa kweli wa taifa na maridhiano ya dhati yanaweza kupatikana tu kupitia uchunguzi huru, wa kuaminika na ulio wazi,” amesema.
Maharagande amesema wameshangazwa kusikia kuwa, baada ya Tume ya Jaji Chande, sasa kutaundwa tume nyingine kufanya uchunguzi wa kijinai wa matukio yale yale.
Amesema huo ni ujanja mwingine wa kupoteza muda na kutafuna fedha za walipa kodi, akisisitiza kuwa Watanzania hawawezi kukubali ulaghai wa aina hii.
Amesema ACT Wazalendo inarudia wito wake wa kuundwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa chini ya taasisi zenye kuaminika kama Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika au SADC.
“Hii ni kauli yetu ya awali, msimamo wa kina zaidi utakaoangazia maeneo yote utatolewa baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya Chama Taifa kitakachoketi hivi karibuni ndani ya kipindi cha wiki moja,” amesema.