Tabora. Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella ameongoza shughuli ya kusafisha Barabara ya Usule iliyopo Kata ya Mbugani Manispaa ya Tabora, ambayo imekuwa ikitajwa kama eneo la mauaji ya waendesha bodaboda na kuporwa kwa pikipiki zao.
Barabara ya Usule ina miti mingi mikubwa ya miembe katika pande zote mbili, hivyo kutengeneza giza nene ambalo linatajwa kutumiwa na wahalifu kujificha.
Katika usafi huo ulioshirikisha makundi ya vijana, waendesha bodaboda na wananchi, matawi ya miti hiyo yamepunguzwa na vichaka vya pembezi kufyekwa ili eneo liwe wazi.
Akizungumza na wananchi leo Aprili 24, 2026, Wella amesema pamoja na usafi huo, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuimarisha ulinzi, ikiwa ni pamoja na kuendesha operesheni mbalimbali.
Mkuu wa wilaya ya Tabora, Upendo Wella akizungumza na wananchi wa kata ya Mbugani baada ya kukamilika kwa zoezi la usafishaji wa barabara ya Usule katani humo.
“Hili zoezi ni la awali tu, tunaendelea kuhakikisha tunatokomeza uhalifu katika maeneo haya wananchi wafanye shughuli zao kwa amani na utulivu badala ya kuwa na hofu na njia,” amesema Wella.
Amewaonya wakazi wa Usule kuacha tabia ya kuwapokea wageni wasiowajua, ambao hata kwenye uongozi wa serikali ya mtaa wao hawafahamiki, kwa kuwa ni chanzo cha uhalifu na wengi wamefanya matukio kisha kukimbilia kusikojulikana.
“Hapa Usule pia kuna wageni wengi kwa taarifa nilizo nazo, sasa ndugu zangu hilo nalo ni tatizo na najua Watanzania tuna roho nzuri kwamba mtu akiomba msaada mnatoa haraka lakini wengine sio wema,” amesisitiza.
Aidha, baada ya shughuli hiyo Wella amesikiliza na kutatua kero za wananchi ambapo Adam Issa mkazi wa Usule amesema kwenye Kata ya Mbugani hakuna zahanati wala kituo cha afya, hali inayowalazimu kwenda kata nyingine kupata huduma na kuwa likitokea tatizo usiku wa manane kwao inakua changamoto.
“Hawa wahalifu mara nyingi wanafanya matukio usiku, sasa wakati mwingine unakuta mtu umepata mgonjwa usiku inabidi upite hilo pori uende hospitali ndiyo maana tunaumizwa,” anasema Issa.
Amesema mwaka jana kuna mwanamke mmoja mgonjwa alikuwa na mume wake wanaenda hospitali usiku akabakwa na wahalifu mbele ya mume wake licha ya kuwa mgonjwa. Hii ni kwa sababu Mbugani hakuna zahanati huduma za afya zinafuatwa maeneo mengine.
Wananchi wa kata ya Mbugani wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Tabora Upendo Wella
“Tuko hapa mjini kabisa lakini huduma tunafuata mbali, hatupendi kutoka usiku ila inatulazimu kama hivyo mtu kaumwa usiku inabidi utoke hakuna jinsi,” amesema.
Katika majibu yake mkuu wa wilaya amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote, hivyo hata Mbugani itapata huduma hiyo ni suala la muda mfupi tu kwa kuwa Serikali haiko tayari kuona wananchi wake wanateseka.
“Tunakwenda kwa awamu lakini niwaambie tu wananchi wote huduma muhimu zitawafikia ni hatua kwa hatua kama hivi mnaona tuna madarasa mazuri lakini hata maeneo ambayo zahanati zimekamilika ziko vizuri, kwa hiyo hata sisi tutanufaika karibuni,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa waendesha Bodaboda Mkoa wa Tabora, Mrisho Shime amemwomba mkuu wa wilaya maafisa maendeleo ya jamii waendelee kutoa elimu ili vijana watambue fursa walizo nazo ili kupunguza uhalifu Tabora.
“Kuna wakati fursa tunazo lakini hatujui kama ni fursa lakini wenzetu kwa kuwa wamesomea haya mambo wanaweza kutusaidia sana.
Kata ya Mbugani ni miongoni mwa kata 29 zinazounda halmashauri ya manispaa ya Tabora ambapo licha ya kuwa mjini, bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma muhimu kama vile zahanati, kituo cha Polisi, soko na huduma nyinginezo.