Roma, Italia. Shirikisho la Soka Italia (FIGC) linafikiria kufanya jaribio la kumshawishi Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Italia kufuatia kuondoka kwa Gennaro Gattuso.

Gattuso aliondolewa mapema mwezi huu baada ya kushindwa kuiongoza Italia kufuzu Kombe la Dunia, hali iliyosababisha mshtuko mkubwa juu ya mustakabali wa soka la nchi hiyo.

Baada ya kipigo cha penalti dhidi ya Bosnia katika mechi ya mtoano, rais wa FIGC, Gabriele Gravina, alijiuzulu, huku pia gwiji wa makipa Gianluigi Buffon akiondoka katika nafasi yake ya Mkuu wa Wajumbe wa timu ya taifa.

Ndoto ya Guardiola

Licha ya sintofahamu iliyopo, vyombo vya habari vya Hispania vinaripoti kuwa Italia ina ndoto ya kumshawishi Guardiola kuondoka Manchester City na kuanza enzi mpya na Azzurri.

Taarifa zinaeleza kuwa kocha huyo ana mkataba wa mwaka mmoja uliobaki Manchester City, lakini mustakabali wake baada ya hapo bado haujaeleweka.

Kwa mujibu wa ripoti, Guardiola yuko tayari kusikiliza ofa kutoka Italia iwapo itawasilishwa, ingawa dili hilo linaonekana kuwa gumu kifedha.

Kikwazo cha mshahara

Guardiola anaripotiwa kulipwa takribani euro 24.8 milioni (Sh76 bilioni) kwa mwaka huko Etihad kiasi kikubwa mno ukilinganisha na makocha wa timu za taifa.

Kwa mfano, kocha aliyewahi kuipa Italia ubingwa wa Euro 2020, Roberto Mancini, alipata karibu euro milioni tatu (Sh9 bilioni) kwa mwaka.

Hata hivyo, changamoto hizo hazijamzuia beki wa zamani wa Italia, Leonardo Bonucci, kuunga mkono wazo hilo.

“Tungeanza upya na Guardiola. Ndiye mtu sahihi kwa Italia. Najua si rahisi, lakini kuota hakugharimu,” amesema Bonucci.

Guardiola mwenyewe anasema nini?

Guardiola mwenyewe amewahi kueleza kuwa anatamani kufundisha timu ya taifa siku zijazo.

“Napenda kupata uzoefu wa Kombe la Dunia au Euro. Sijui lini labda baada ya miaka mitano au zaidi lakini ningependa kufundisha kwenye mashindano makubwa ya kimataifa,” aliwahi kusema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *