Big Catch-Up ambao ni mpango wa kimataifa wa kuhakikisha hali ya utoaji wa huduma za chanjo muhimu kwa watoto duniani iliyodorora kufuatia janga la coronavirus“>COVID-19 inarejea kawaida,  umefanikiwa kutoa zaidi ya dozi milioni 100 za chanjo kwa watoto duniani, yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile afya, WHO na la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na Ubia wa chanjo duniani, GAVI.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa tarehe 24 Aprili 2026 kutoka Geneva, Uswisi  na New York Marekani, mashirika hayo yamesema mpango huo uliowezesha kuwafikia takribani watoto milioni 18.3 katika nchi 36, ulilenga kuongeza upatikanaji wa chanjo na kupunguza pengo la usawa wa huduma za afya kwa watoto walio hatarini zaidi.

Taarifa hiyo imetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Chanjo duniani iliyoanza leo Aprili 24 hadi Aprili 30.

media:entermedia_image:a8018f3e-a909-4cb4-9fdd-e9611f131b1e

© UNICEF/Johnny Shahan

Joud, 3, anapokea chanjo katika kituo cha afya cha Saqba wakati wa kampeni ya kitaifa ya chanjo huko Damascus Vijijini, Syria.

Mafanikio makubwa ya mpango wa chanjo

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mafanikio ya mpango wa Kampeni Kubwa ya Kufidia Chanjo” au Big Catch-Up ni pamoja na:

  • Watoto milioni 18.3 kufikiwa na huduma za chanjo
  • Kufikia takribani watoto milioni 12.3 waliokuwa hawajawahi kupata chanjo kabisa chanjo.
  • Watoto milioni 15 kupatiwa chanjo dhidi ya Surua
  • Dozi milioni 23 za chanjo ya ugonjwa wa kupooza au Polio (IPV) kutolewa

Mashirika hayo yamesema hatua hiyo ni muhimu katika juhudi za kimataifa za kutokomeza magonjwa ya kuambukiza na kulinda maisha ya watoto.

Mtoto akipatiwa chanjo Gaza, kampeni inayoungwa mkono na WHO

© UNRWA/Ashraf Amra

Mtoto akipatiwa chanjo Gaza, kampeni inayoungwa mkono na WHO

Sababu ya kuanzishwa kwa mpango

Sababu ya kuanzishwa kwa mpango

Mpango huo ulianzishwa mwaka 2023 ili kukabiliana na kushuka kwa viwango vya chanjo duniani, hasa kutokana na athari za janga la COVID-19 ambalo liliathiri mifumo ya afya na huduma za msingi.

Aidha, ulilenga kuwafikia watoto waliokosa chanjo katika umri mdogo, wakiwemo wale wenye umri wa miaka 1 hadi 5 ambao hawakuwahi kufikiwa na huduma hizo awali.

Pengo la chanjo bado ni changamoto

Licha ya mafanikio hayo, mashirika hayo yameonya kuwa changamoto bado ipo, yakibainisha kuwa:

  • Takribani watoto milioni 14.3 chini ya mwaka mmoja hawakupata chanjo yoyote mwaka 2024
  • Visa vya surua vilifikia takribani milioni 11 mwaka huo
  • Idadi ya nchi zilizoathirika na milipuko ya surua imeongezeka mara tatu tangu 2021

Hali hii inaonesha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kawaida ya chanjo ili kuhakikisha ulinzi wa kudumu kwa watoto.

Wafanyakazi wa kujitolea wa afya ya jamii wakitoa chanjo ya kipindupindu kwa watu katika soko moja la kusini magharibi mwa Kenya.

© GAVI/Kelvin Juma

Wafanyakazi wa kujitolea wa afya ya jamii wakitoa chanjo ya kipindupindu kwa watu katika soko moja la kusini magharibi mwa Kenya.

Tanzania na Kenya miongoni mwa nchi zilizopata mafanikio

Nchi kadhaa, hasa barani Afrika na Asia, zimepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango huo, zikiwemo:

  • Burkina Faso
  • Ethiopia
  • Kenya
  • Somalia
  • Tanzania
  • Zambia

Nchi hizi zimefanikiwa kuwafikia zaidi ya asilimia 60 ya watoto waliokuwa hawajapata chanjo ya msingi ya chanjo dhidi ya Dondakoo, Pepopunda, na Kifaduro(DTP1).

Wito wa kuimarisha uwekezaji

Mashirika hayo yamesisitiza kuwa juhudi za kurejesha chanjo zinapaswa kuendelea sambamba na uwekezaji wa muda mrefu katika mifumo ya afya ili kuhakikisha huduma za chanjo zinawafikia watoto wote bila kukatizwa.

WHO, UNICEF na GAVI zilitoa chanjo za COVID-19 na nyinginezo kwa jamii za mbali katika Visiwa vya Solomon mwaka wa 2022. (Maktaba)

© WHO/Neil Nuia

WHO, UNICEF na GAVI zilitoa chanjo za COVID-19 na nyinginezo kwa jamii za mbali katika Visiwa vya Solomon mwaka wa 2022. (Maktaba)

Katika kuadhimisha Wiki ya Chanjo Duniani 2026, wadau wamezindua kampeni ya “Kwa Kila Kizazi, Chanjo Hufanya Kazi,” wakihimiza nchi kuongeza juhudi za kulinda afya ya watoto na kuzuia milipuko ya magonjwa.

WHO na washirika wake wamehitimisha kwa kusisitiza kuwa chanjo ni moja ya njia bora zaidi za kuokoa maisha, na kwamba hakuna mtoto anayepaswa kuachwa bila ulinzi dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *