Dar es Salaam. Ibada katika uislamu ni upeo wa mwisho wa kunyenyekea na ukomo wa ndani wa hisia kwa utukufu wa yule unayemuabudu.

Ni daraja la mawasiliano, ni nguzo ya uhusiano kati ya kiumbe na Muumba wake. Ni uhusiano wa kiutendaji kati ya Allah Mtukufu na viumbe wake.

Katika Uislamu, maisha ya mtu  yote huwa ni ibada na hivyo ni lazima uhai wa mtu  wote uwe ni  kwa ajili ya kumtii Allah katika kila kipengele cha maisha yake  ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, kisiasa na vipengele vinginevyo vyote.

Na hii ndiyo maana halisi ya maneno ya Allah anaposema: ‘’Na sikuwaumba watu na majini isipokuwa kwa ajili ya kuja kuniabudu, sitaki kutoka kwao chakula na sitaki kutoka kwao wanilishe [mimi sina sifa hizo] Hakika Allah yeye ni mtoaji wa rizk na ni mwenye nguvu kubwa na madhubuti sana” [ Quran 55:57-58]

Pia anasema: “Sema ewe mja hakika swala zangu na ibada zangu na uhai wangu na kufa kwangu, yote haya ni  [na mengine] ni miliki ya Allah mlezi wa viumbe wake” (Quran 6:166).

Ili Muislamu adumu kwenye ibada na ahisabike yumo kwenye ibada, anapaswa kuzingatia yafuatayo;

Moja,  ziwe ibada zake zote ni hai na zenye uhusiano wa kweli na Muumba. Yaani unapasa kufanya ibada kwa ajili yake Mwenyezi Mungu na ufanye hivyo kana kwamba unamuona. Na hii ndiyo maana ya ‘Ihsan’

Mtume aliulizwa kuhusu Ihsani akasema; ”Ni kumuabudu Allah kama unamuona na kama wewe humuoni, elewa yeye anakuona.”

Mbili, Ibada zifanywe kwa unyenyekevu. Unapaswa kuhisi kuwa kama upo kwenye swala, basi Allah  yuko mbele yako anakusimamia katika ibada yako. Ukiwa na hisia hii basi utajenga khushui (unyenyekevu) kwake

Ili kupata unyenyekevu, unapaswa kuuhudhurisha moyo wako ndani ya swala zako kwa kuachana na fikra za kidunia. Mtume anasema (rehma zimshukie): ‘’Allah haangilii swala ya yule mtu ambaye katika swala yake hahudhurishi moyo wake pamoja na mwili wake. Tunafundishwa kuwa unyenyekevu sio wa moyo tu bali pia mwili wako unapaswa kuwa na utulivu wa hali ya juu.

Tatu, kukithirisha kufanya ibada za swala zikiwamo swala za sunna.

Katika Hadithi Qudusiyyi, Mtume (rehma zimshukie) anasema: Allah anasema yeyote atakayetaka kumuudhu kipenzi changu [walii] hakika mimi nimemtangazia vita kati yangu na yeye, Hatojikurubisha  kwangu mja wangu kwa swala za sunnah mpaka mimi nitampenda, pindi mimi nitakapompenda basi mimi ndiye nitakuwa sikio lake la kusikilizia, na nitakuwa  macho yake  ya kutazamia, na mkono wake wa kushikia na  mguu wake  wa kutembelea. Na pindi akiniomba mimi chochote hakika nitampa yeye alichokiomba, Na pindi akiniomba ulinzi hakika nitamlinda yeye, Na kama atasitasita mja wangu kufanya chochote basi mimi nitamfanyia badala yake kile alichokisita kukifanya..’’

Miongoni mwa swala za sunna zilizohimizwa sana ni kusimama usiku kuswali. Swala hii ni chemichemi inayozalisha imani ya kweli mioyoni mwa waumini.

Allah anasema hakika kisimamo cha usiku ni chenye nguvu na ndicho chenye kumuandaa mja kiimani na ndicho chenye kumfanya mja kuwa na kauli yenye nguvu. [ Quran: 74:6].

Hakika amewasifu Allah waja wake waumini kwa kauli yake kuwa walikuwa wanalala kidogo usiku, na kusimama sana kuswali swala za usiku.

Sasa tuone baadhi ya ibada ambazo Muislamu anapaswa kudumu nazo maishani. Hizi ni pamoja na  kisimamo cha usiku kila siku,  swala ya tarawehe, kufunga kila Jumatatu na Alhamisi,  funga ya Arafa kwa wasioenda Hijja na  funga ya siku ya Ashuraa. (mwezi Muharram)

Nyingine ni funga ya siku sita katika mwezi wa Shawali,  Funga ya siku nyeupe yaani tarehe   13 hadi 15 kila mwezi katika kalenda ya Kiislamu na kufanya Itkafu muda wowote na siku yoyote.

Ibada ya kusoma Quran

Hii ni ibada kubwa sana katika Uislamu hasa ikisomwa kwa mazingatio na kuelewa kinachosomwa.

Tunatakiwa kuisoma Qur kwa mazingatio, unyenyekevu na kwa huzuni. Mtume (rehma zimshukie) anasema: ‘’Hakika hii Qur an imeshushwa katika mazingira ya huzuni, basi mtakapoisoma huzunikeni.

Pia anasema kuwa watu walio bora katika ummah wangu ni wale wanaoisoma Qur an. Na katika hadith ya Ibnu Masoud kutoka kwa Mtume (rehma zimshukie) kasema:” Hakika hii Q ur an ni adabisho la Allah,  basi ikubalini hii Qur an ambayo ni adabisho lake kwa kiwango chenu cha uwezo wenu.’’

Pia, hii Qur an ni nuru  kuu na ni ponyo lenye manufaa kwa yeyote mwenye kushikamana nayo na ni mwokozi kwa mwenye kuifuata.

 Hatapotoka mtu yeyote isipokuwa Qur an itamnyoosha, na hatopinda mtu isipokuwa Qur an itamnyoosha vizuri.

Mtume (rehma zimshukie) alimuusia sahaba wake mmoja aitwaye Abuu Dharr akimwambia: ‘’Ni juu yako kuisoma Qur an, Hakika hii Qur an ni nuru yako katika hii ardhi na ni kiombezi chako huko akhera.

Ukisoma Quran utalipwa ujira kwa kila herufi unayoisoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *