Dar es Salaam. Shirika la Bahari Duniani (IMO) limezitaka nchi za Afrika kuharakisha utekelezaji wa mfumo wa dirisha moja la kidijitali la uondoshaji wa mizigo bandarini, likieleza kuwa hatua hiyo ni ya lazima kuongeza ufanisi wa bandari na ushindani wa kiuchumi.
Mfumo huo hurahisisha uingizaji na uondoshaji wa mizigo bandarini kwa kupunguza matumizi ya nyaraka, zinazozungushwa na wateja taasisi mbalimbali wakati wa kufuatilia au kuagiza mizigo.
Hayo yameelezwa leo Aprili 24, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Bahari Afrika wa IMO, Mwanaulu Mwajita, wakati akizungumza katika hafla ya kufunga mkutano wa kimataifa wa mafunzo kuhusu usafirishaji wa majini.
Mkutano huo uliandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) kwa kushirikiana na Benki ya Duniani, IMO, Shirika la SSTP Afrika pamoja na Korea World Bank Fund.
Washiriki mbalimbali wa Mkutano wa kimataifa wakiwa katika mafunzo kuhusu usafirishaji wa majini uliofanyika Dar es Salaam, Aprili 24, 2026.
Mwanaulu amesema utekelezaji wa lazima wa mfumo wa dirisha moja la kidijitali katika utoaji wa huduma bandarini ulianza kutekelezwa Januari 2024, na kwamba mfumo huo ni muhimu kurahisisha huduma za bandari.
Amesema mfumo huo, unaoendana na mkataba wa kurahisisha usafirishaji wa Majini wa IMO, unasaidia kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na kuimarisha ushindani wa bandari za Afrika katika soko la kimataifa.
“Warsha hii imeonyesha wazi kuwa mabadiliko kuelekea mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za bandari si chaguo tena, bali ni hitaji la lazima,” amesema.
Hata hivyo, amesema licha ya hatua zilizopigwa na baadhi ya nchi, bado kuna haja ya kuimarisha uratibu wa kitaifa kati ya taasisi mbalimbali, kuoanisha mifumo ya kisheria na kidijitali, pamoja na kuwekeza katika mifumo inayoweza kuwasiliana.
Awali, akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis, amesema mageuzi ya kidijitali katika sekta ya bandari ni hatua ya lazima itakayobadilisha ushindani wa biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Amesema mwelekeo wa dunia sasa umejikita katika matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kurahisisha shughuli za bandari, kupunguza ucheleweshaji na kuongeza uwazi katika mnyororo mzima wa biashara.
“Ushirikiano wa kikanda na kimataifa ndio msingi wa mafanikio ya mabadiliko haya; hakuna nchi inayoweza kufanikiwa peke yake,” amesema Khamis.
Ameongeza kuwa Tanzania inalenga kujenga sekta ya bahari iliyo ya kisasa, jumuishi na inayotumia teknolojia kusaidia ukuaji wa uchumi, akisisitiza kuwa mifumo jumuishi ya kidijitali itarahisisha mtiririko wa bidhaa, huduma na taarifa kwa ufanisi zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Zanzibar, Akif Ali Khamis akizungumza wakati akifunga mkutano wa kimataifa wa mafunzo kuhusu usafirishaji wa majini uliofanyika Dar es Salaam.
Khamis amesema sekta ya usafiri wa majini ina nafasi muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya kujenga uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza kipato cha mwananchi, hivyo uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ni muhimu.
“Utekelezaji wa mifumo ya kidijitali bandarini ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha biashara na kuongeza ushindani wa uchumi wa taifa. Bila mifumo inayoweza kuwasiliana, hatuwezi kufikia faida kamili ya mageuzi ya kidijitali,” amesema.
Akielezea dhamira ya mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum amesema lengo la mkutano huo lilikuwa kujenga uelewa wa pamoja kwa nchi za Afrika kuhusu umuhimu wa kuanzisha mfumo wa dirisha moja la kidijitali la uondoshaji wa mizigo bandarini.
Amesema uwepo wa mfumo huo ni utekelezaji wa mkataba wa kimataifa unaotaka nchi wanachama kuwa tayari kuutumia kuanzia Januari 2024.
“Mafunzo haya yameangalia hali ilivyo katika nchi za Afrika na kutoa mwongozo wa mambo muhimu yanayohitajika katika utekelezaji wa mfumo huo,” amesema.
Salum alisema baada ya mkutano huo, kila nchi itafanya tathmini ya hali yake katika utekelezaji wa mfumo huo, huku changamoto kubwa iliyobainika ikiwa si fedha, bali ni mazoea ya kutumia mifumo ya zamani.
“Tanzania tuna bahati kuwa tayari tumefanyiwa tathmini na kupata ripoti ya hali halisi. Sasa tunaweka mikakati ya utekelezaji, hivyo tumenufaika kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Aliongeza kuwa uwepo wa mfumo mmoja wa taarifa utarahisisha biashara kwa kuharakisha uingizaji na uondoshaji wa mizigo pamoja na huduma za meli bandarini.