Sitisho hilo lilianza kutekelezwa tarehe 16 Aprili kufuatia mazungumzo ya nadra ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili, ya kwanza katika zaidi ya miongo mitatu.

Ingawa hatua hiyo inaleta matumaini ya kupungua kwa mvutano, Umoja wa Mataifa unaonya kuwa hali ya kibinadamu bado ni mbaya.

Athari kwa raia na wakimbizi zazua wasiwasi-OHCHR

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR, zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Lebanon kutokana na mashambulizi na maagizo ya kuhama.

Msemaji wa ofisi hiyo ya Haki za binadamu Thameen Al-Kheetan amesema mashambulizi mengi ya Israel yalifanyika bila tahadhari ya kutosha kwa raia.

“Katika mashambulizi mengi ya Israel, hakukuwa na onyo, au hakukuwa na onyo lenye ufanisi, jambo lililowazuia raia wengi kuondoka kwa usalama,” amwsema.

Ameongeza kuwa maagizo mengi ya kuhama yanayohusu karibu asilimia 14 ya eneo la Lebanon yanaweza kufikia kiwango cha ufurushwaji wa kulazimishwa, jambo lililokatazwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu, akisisitiza kuwa raia wanapaswa kuruhusiwa kurejea nyumbani kwa usalama.

Mfanyakazi anaendesha forklift katika ghala, akisafirisha pallets za misaada ya chakula iliyoandikwa 'Imefadhiliwa na Msaada wa Kibinadamu wa Jumuiya ya Ulaya'. Hii ni sehemu ya hisa ya tani 1,000 inayowasili kwenye ghala la WFP huko Beirut, Lebanon.

© WFP/Mustapha Ghabris

Vyakula vya tayari-kula vilivyochangwa na ECHO vilivyowasili hivi karibuni vimepakiwa kwenye ghala la WFP huko Beirut, Lebanon.

Mashambulizi dhidi ya raia na huduma muhimu yakosolewa

Umoja wa Mataifa pia umeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi yanayolenga wahudumu wa afya na wanahabari. Shambulio la hivi karibuni lilimuua mwanahabari wa Lebanon Amal Khalil na kumjeruhi mpiga picha Zeinab Faraj, huku vikosi vya uokoaji vikidaiwa kushambuliwa walipokuwa wakijaribu kufika eneo la tukio.

“Wahudumu wa afya, iwe wa kijeshi au kiraia, pamoja na raia wengine wakiwemo wanahabari, wanalindwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu. Kuwalenga kwa makusudi kunaweza kuwa uhalifu wa kivita,” amesisitiza Al-Kheetan.

Ripoti nyingine ya Umoja wa Mataifa inaeleza uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu, huku familia nzima zikiripotiwa kupoteza maisha katika mashambulizi, na pia mashambulizi ya makombora kutoka Lebanon kuelekea maeneo ya makazi nchini Israel.

Kifo cha mlinda amani chaonesha hatari zinazoendelea

Hata wakati juhudi za kidiplomasia zinaendelea, hatari kwa wafanyakazi wa kimataifa bado ni kubwa.

Mpango wa Mpitio wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL umethibitisha kifo cha mlinda amani mwingine kutoka Indonesia, Koplo Rico Pramudia, aliyefariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika mlipuko kwenye kambi yake kusini mwa Lebanon.

Ujumbe huo umetoa pole kwa familia yake na kusisitiza uwajibikaji .

Mashambulizi dhidi ya walinda amani ni “ukiukwaji mkubwa ambao unaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kivita,” imesema UNIFIL, ikizitaka pande zote katika mzozo kuheshimu sheria za kimataifa na kulinda wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

FAO na serikali washirikiana kufufua shughuli za kilimo

Wakati huo huo, juhudi za kuimarisha maisha zinaendelea, ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAI, linashirikiana na Wizara ya Kilimo ya Lebanon kusaidia kurejesha mifumo ya kilimo katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro kusini mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaonya kuwa kuongeza muda wa sitisho la mapigano pekee hakutoshi kumaliza mgogoro huu.

Kama alivyoeleza Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, uchunguzi huru na wa kina kuhusu ukiukwaji unaodaiwa kufanyika ni muhimu wakati mamilioni ya watu bado wanasubiri amani ya kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *