Katika mji wa Nasir walinda amani wa UNMISS wanaendelea kushika doria, wakitoa hakikisho la usalama huku familia zikirejea katika mji wao uliosambaratika. Athari za mapigano bado zinaonekana bayana, lakini pia uthabiti wa wakazi wake.

Katika nyakati chache za furaha, jamii hukusanyika kuimba na kucheza ikiashiria kurejea kwa utulivu, japo kwa tahadhari. Samuel Gai ni ni kiongozi wa kijamii hapa Nasir

“Nilikuwa na hofu kurejea wakati mapigano yalipoanza. Hata sasa, nimerudi nikiwa na wasiwasi. Lakini kama mzee, niliona ni lazima nirejee na naamini wengine watafuata.”

Wanawake na watoto ni miongoni mwa wanaoongoza kurejea wakifungua tena nyumba, kurejesha shughuli za kila siku, na kufufua biashara ndogo ndogo.

Kwa baadhi yao, usalama ulioboreshwa tayari unaleta fursa za kiuchumi ikiwemo kwa Sara Galtluak mkazi wa hapa Nasir,

“Mimi ni mfanyabiashara hapa Nasri ,ninaendesha mgahawa wa chakula na chai na biashara nyingine ndogo ndogo hapa. Kwa sababu kuna utulivu sasa, ninaweza kupata faida. Amani hii inatusaidia kusonga mbele.”

Mamlaka za eneo na maafisa wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi kwa karibu na jamii wakizingatia ulinzi, maridhiano, na mnepo wa muda mrefu.Marwa Yousif ni afisa wa UNMISS anayeshughulikia Ulinzi, Mpito na Urejeshaji wa Jamii

“Ni muhimu juhudi mbalimbali zifanyike mashinani. Sio tu kushirikiana na mamlaka, bali pia kuwahusisha viongozi wa jamii na vijana, ili kuimarisha mitandao ya ulinzi na mshikamano wa kijamii.”

Hata hivyo, safari ya kujikwamua haikosi kumbukumbu za machungu. Ibada ya kumbukumbu imefanyika kuwaenzi  waliopoteza maisha akiwemo mfanyakazi wa helikopta ya Umoja wa Mataifa aliyeuawa wakati wa mapigano.

Kando ya Mto Sobat, maisha yanaendelea kusonga ikiwa ishara ya uvumilivu kwa jamii inayojijenga upya, hatua kwa hatua.
na licha ya changamoto zilizobaki, kurejea kwa wakazi wa Nasir kunatoa matumaini mapya ya amani ya kudumu nchini Sudan Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *