Kwa mujibu wa takwimu za mamlaka ya Palestina, zaidi ya asilimia 80 ya watu hawana ajira wakati huo huo bei za bidhaa muhimu zikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 37, hali hii ngumu imewaweka wana Gaza katika kile kinachoitwa “uchumi wa kujikimu” au survival economy.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa aliyeko Gaza alitembelea masokoni na kuzungumza na vijana waliokuwa chuo kikuu kabla ya vita na wahitimu ambao walikuwa na ndoto za maisha bora lakini sasa wanajikuta wakifanya kazi ambazo hazilingani na taaluma zao.
Abdullah Al-Khawaja, mhitimu wa uhandisi wa umeme, anafanya kazi kama muuzaji wa viungo vya chakula kwenye barabara ya Khan Younis.
Wa kwanza ni Abdullah Al-Khawaja, mhitimu wa uhandisi wa umeme, ambaye alilazimika kuhama kutoka Rafah hadi Khan Younis, sasa anauza viungo kwenye kibanda kidogo sokoni.
“Baada ya miaka mingi ya mateso wakati wa masomo ya chuo kikuu, tulikuwa na ndoto na matarajio ya kufikia malengo yetu na kufikia maeneo ambayo yangetuletea furaha na kutimiza matarajio yetu yote. Lakini baada ya kuzuka kwa vita, ndoto zote ziliharibiwa, na kila njia kuelekea matarajio yetu ilifutika. Tulijikuta tumesimamishwa kati ya mbingu na dunia, hatuwezi kufikia malengo yetu au hata kurudi mwanzo. Kwa hivyo, tumelazimika kugeukia kile kwenye ‘uchumi wa kujikimu.’ Kwasas tunajaribu kutafuta fursa za ajira. Nilipata moja, lakini haifikii matarajio yangu kama mhitimu mchanga mwenye sifa za kitaaluma.”
Ayham Al-Najjar anafanya kazi katika kibanda cha kuuza peremende na vinywaji huko Khan Younis, Gaza.
Katika soko hilo hilo, Ayham Al-Najjar, ambaye alitamani kuwa mhasibu, sasa anauza vinywaji, biskuti na pipi.
“Nilikuwa na ndoto ya kumaliza chuo, kupata kazi na kujenga nyumba na maisha mazuri. Lakini vita vilitushtua. Niligeukia kufanya kazi kwenye kibanda ili kupata riziki na kuisaidia familia yangu. Vita vilitushtua.”
Huyu hapa ni Mustafa Salouh, yeye anauza sabuni za kuogea na za usafi.
“Mimi ni mhitimu wa chuo kikuu, na nilikuwa na ndoto za maisha bora kuliko hali halisi ya sasa. Kwa sababu ya vita, tuliishi katika kipindi cha kusikitisha. Sasa tunakaa kwenye kibanda ili kujikimu sisi na familia zetu. Tunaishi maisha ambayo hatujawahi kufikiria, hali halisi ambayo hatuwezi hata kuielezea.”
Mustafa Sadiq naye ana hadithi kama hiyo. Kwa sasa anauza vitabu na vifaa vya shule baada ya mipango yake ya elimu na taaluma kusambaratika.
Mustafa Sadiq huuza karatasi na vitabu vya elimu katika kibanda chake katika Soko la Khan Younis huko Gaza.
“Matarajio yangu yalikuwa makubwa sana. Lengo langu lilikuwa kukamilisha masomo yangu ya chuo kikuu na kufikia kile nilichokuwa nimepanga kwa ajili ya mustakabali wangu. Lakini kwa bahati mbaya, miaka mitatu ya maisha yetu ilipotea, na sasa tunalazimika kukaa kwenye kibanda. Namshukuru Mungu, bado tupo hai.”
Simulizo zote hizo zinathibitisha suala moja muhimu, hali ngumu ya kiuchumi inayoendelea kuzorota katika Ukanda wa Gaza, ambapo wakazi wengi sasa wanahangaika kupata mahitaji ya kila siku kutokana na ukosefu wa ajira.