Ukame umesababisha watu zaidi ya 62,000 kuyahama makazi yao katika wilaya tano nchini Somalia, tangu kuanza kwa mwaka huu, huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa hali ya nchi nzima, inaweza kuwa mbaya.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Umoja wa Mataifa, inayoshughulikia wahamiaji, inasema, hali ni mbaya katika wilaya hizo tano za Baidoa, Dayniile, Kahda, Diinsoor na Doolow kati ya 90 ambazo zilichunguzwa, na hali inaonesha kuwa wakaazi wake wanakabiliwa na baa la njaa.

Aidha, Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa ukame huo umesababisha mimea kukauka mashambani na hivyo, wakaazi kukosa chakula, huku ikihofia kuwa idadi ya watu waliothirika nchi nzima, inaweza kufikia zaidi ya 300,000.

Hata iwapo kutakuwa na mvua kati ya mwezi Aprili na Juni, watu wengine 125,000 wanakadiriwa kuwa huenda wakayakimbia makaazi yao kwa sababu ukame utaendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi.

Mbali na mimea kukauka, kuna uhaba wa maji ya kunywa kwa binadamu na mifugo, hali ambayo imesababisha wafugaji kuhamia maeneo mengine kutafuta malisho na chakula.

Mwezi Februari, wataalam wa Umoja wa Mataifa walionya kuwa, idadi ya watu wanaokabiliwa na uhaba wa chakula nchini Somalia, imeongezeka na kufikia Milioni 6.5, na kukadiria kuwa watoto zaidi ya Milioni 1.8 wapo kwenye hatari ya kusumbuliwa na utapiamlo kwa kukosa lishe bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *