Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuwasilishwa ripoti ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi, wadau wameibua mitazamo tofauti, baadhi wakiiona kama mwanzo wa tumaini la mwafaka kitaifa, wengine wakisema haijakidhi matarajio.
Tume ya uchunguzi wa matukio hayo iliyoongozwa na Jaji Othman Chande, ilikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan juzi, ikianisha mambo mbalimbali ikiwamo vyanzo na vichocheo vya vurugu pamoja na mapendekezo.
Rais Samia naye, alisema ripoti hiyo imesaidia kuuonyesha ukweli, katikati ya shutuma na kunyooshewa vidole kulikoikabili Tanzania, huku akieleza angetamani kurudisha siku nyuma ili ghasia hizo zisitokee kuichafua historia ya Tanzania.
Licha ya baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani kuipinga na kuikosoa ripoti hiyo, wengine, wamesema imekidhi matarajio kwa kuwa imegusa maeneo yote, huku wakiitaja kuwa mwanzo mpya wa safari ya kujenga maridhiano na hatimaye mshikamano wa kitaifa.
Msimamo wa kuipinga, mbali na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichokosoa juzi uhalali wa Tume yenyewe, vilevile umetolewa na Chama cha ACT Wazalendo, kikisema hitimisho la Tume hiyo lilitarajiwa kutokana na muundo wake, wajumbe wake na hadidu za rejea ilizopewa kufanyia uchunguzi.
“ACT Wazalendo tunaombeleza kila maisha yaliyopotezwa na kila familia iliyopata madhila kufuatia matukio ya tarehe 29 Oktoba na athari zake. Uponyaji wa kweli wa taifa na maridhiano ya dhati yanaweza kupatikana tu kupitia uchunguzi huru, wa kuaminika na ulio wazi,” imesema taarifa ya chama hicho iliyosainiwa na Mbarala Maharagande, naibu katibu wa haki za binadamu na vyombo vya uwakilishi wa wananchi.
Chama hicho, kimeeleza kushangazwa na ahadi ya kuundwa tume nyingine ya kufanya uchunguzi wa kijinai wa matukio hayohayo yaliyochunguzwa na tume ya Jaji Chande.
“Hii ni kauli yetu ya awali, msimamo wa kina zaidi utakaoangazia maeneo yote utatolewa baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi ya chama Taifa itakayoketi hivi karibuni katika kipindi cha wiki moja,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu ripoti hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema ripoti hiyo imekidhi matarajio kwa kuwa imegusa maeneo yote.
Pia, amesema ripoti hiyo imedhihirisha uwezo wa nchi kusimamia mambo yake, akisisitiza ni ushamba kuamini watu kutoka nje ndiyo wenye uwezo wa kuchunguza ya Tanzania.
“Mmesikia wasifu wa Mwenyekiti wa tume, anaaminika na mashirika ya kimataifa, sasa wakimpa kazi huko sawa sawa, sisi tukipata tatizo tumpe Chande atuchunguzie aaaah hafai, nafikiri hapo wenzetu wanapaswa kufikiria upya,” amesema.
Ameeleza kudhani kuwa uhalali wa tume unatokana na kuwemo kwa mzungu ndani yake ni mtazamo mbaya na hatari.
Alipoulizwa kuhusu ripoti kuitaja kauli ya chama hicho ya ‘Oktoba Tunatiki’ kuwa moja ya vichocheo vya ghasia, amelipinga hilo akisema ghasia zimechochewa na waliowekwa kwenye kambi wakafundishwa kwenda kuvuruga.
Wasira amesema hapingani na maoni ya tume kuwa masuala ya kisiasa, ikiwemo madai ya Katiba Mpya ndiyo chanzo cha ghasia, akidokeza mchakato wa mabadiliko ya Katiba ulianzishwa tangu mwaka 2014.
Lakini, amesema baada ya kufika mbali hadi kuwa na mapendekezo ya mambo yote yanayolalamikiwa, baadhi ya wajumbe wanaounda Ukawa inayohusisha Chadema, CUF na vyama vingine walikimbia mjadala na ndio wanaolalamikia Katiba sasa.
“Kukimbia kwao kulichelewesha kupatikana kwa Katiba. Kumbe wanaosema kupatikana kwa Katiba kumechelewa ndio haohao walioichelewesha na ndio leo wanaidai na mambo yote wanayodai yapo mule kwenye rasimu iliyopendekezwa,” amesema.
Alipoulizwa iwapo wamebaini kuwepo kwa makada wao waliohusika kufadhili ghasia baada ya kukatwa kwenye mchakato ya kugombea, amesema hawezi kuwajua, lakini wakibainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za chama hicho.
Uwajibikaji uzingatiwe
Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya Haki, Amani na Maadili ya madhehebu ya dini, Askofu William Mwamalanga amesema ni muhimu uwajibikaji upewe kipaumbele wakati wa utekelezaji mapendekezo ya tume.
Amesema ni muhimu kuwawajibisha waliokiuka sheria na taratibu za kazi zao, kutaongeza imani ya umma na kuwafanya waone kuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wakosaji.
“Watanzania wasiwe watu wasio waelewa, wanapaswa kuelewa kuwa tume hii ni ya Rais, kama alivyosema mwenyewe, na alipoipokea amekiri hadharani kuwa amesikitika kwa yaliyotokea.
“Pia, ripoti imetoa mapendekezo yake, cha msingi hapa sasa ni uwajibikaji kulingana na yaliyopendekezwa. Nawataka Watanzania wawe watulivu wakati haya yakitekelezwa,” amesema.
Msisitizo wa uwajibikaji, umetolewa pia na Mtaalamu wa sheria, Alloyce Komba aliyesema ili kuwezesha utekelezaji wa mapendekezo ya tume hiyo, suala la uwajibikaji kwa mamlaka zilizohusika ni muhimu.
“Tume ya uchuguzi iliyoundwa na Mandela kule Afrika Kusini ilipowasilishwa, watu walikiri na kuombana msamaha hadharani kabla ya utekelezwaji wa mapendekezo yaliyotolewa,” amesema.
Wahusika wangetajwa
Kwa upande wake, mwandishi na mwanaharakati wa haki za binadamu, Dk Ananilea Nkya anaona kulikuwa na umuhimu ripoti iwataje waliohusika na matukio hayo, hasa ya mauaji ya watu zaidi ya 500.
Kwa mtazamo wake, kutotajwa kwa watu hao, kunafanya hata mapendekezo ya tume yakose nguvu na mjadala, akisisitiza kiu ya umma ni kuwajua wakosaji.
“Kama ripoti haijasema wazi waliohusika na matukio hayo hata hayo mapendekezo ya maridhio na Katiba mpya yanakosa maana,” amesema, akisisitiza kuwa ili hayo yaweze kujadiliwa ni muhimu kuwekwa wazi pande zilizohusika ili kuwezesha majadiliano ya tatizo lililotokea.
Imekidhi hadidu za rejea
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Dk Conrad Masabo, amesema kuhusu kujibu matarajio, tume hiyo haipaswi kuhukumiwa kwa kuangalia mtazamo wa kundi moja bali kwa kuchambua makundi mbalimbali yenye matamanio tofautitoafuti.
“Unapoangalia imejibu matarajio kwa kiwango gani lazima ujue unaongelea matarajio ya nani. Kuna matarajio ya Serikali, matarajio ya wananchi walioumizwa, ambao hawakuumizwa, wanaopigia chapuo Serikali iliyopo na wasiopigia chapuo, yapo pia matarajio ya wadau wa kimataifa. Katika kuchambua matamanio ya jamii na namna yalivyofikiwa lazima tuangalie maeneo hayo,” amesema.
Anafafanua kuwa kwa kuzingatia makundi hayo, si vema kuhukumu kama imekidhi au haijakidhi matarajio; bali kwa maudhui yake, imekidhi matakwa ya hadidu za rejea ilizopewa.
“Kwa Serikali tume imefikia malengo iliyokabidhiwa kuyatekeleza, kwa wananchi walioumizwa sidhani kama imekidhi matarajio yao.”
Amesema ripoti hiyo inasababisha maoni tofauti kwa baadhi ya watu kutokana na msisitizo wake kwenye vichocheo vya vurugu zilizotokea, akisema imejikita kwenye vichocheo badala ya sababu za kutokea kwa vichocheo hivyo.
“Ukishasema chanzo cha vurugu ni Katiba mpya, huwezi kusema mwenye tatizo ni yule aliyeidai bali aliyekwamisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba hiyo.
Kuweka msisitizo kwenye vichocheo ndipo panaibua mjadala hasi kuhusu kipaumbele cha suluhisho kwa wahusika wa kuchunguzwa,” anasema.
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman akisoma Muhtasari wa Ripoti ya Tume hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Aprili 23, 2026.
Kuhusu baraza la wazee, Dk Masabo ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa na utawala, anasema yeye haamini katika baraza hilo, akifafanua mzee wa miaka 80 hawezi kujua changamoto za vijana katika taifa la vijana asilimia 60 ya watu wake.
“Huwezi kuleta wazee kwenye nchi ya vijana wengi uwategemee kufikiri mustakabali wa nchi. Badala ya baraza la wazee, nashauri tuunde baraza kwa uwiano wa watu, vijana wawemo asilimia 60 na wazee waingie kwa uwiano wao kwenye baraza hilo,” anasema.
Akinukuu maneno ya Mwalimu Nyerere aliyewahi kusema, “Taifa liamini vijana hata mkoloni aliamini vijana” anasema vijana wanatakiwa kuhusishwa katika baraza la ushauri wa mwelekeo wa Taifa kwa kuwa wanajua vyema changamoto za sasa na matarajio ya baadaye.
“Kila kundi liwe na baraza lake, tuwe na baraza la vijana, baraza la wazee, baraza la wanawake na ndipo tuunde baraza maalumu la ushauri la Taifa litakalokuwa na uwakilishi wa makundi haya likiwa na uwakilishi sawa wa vyama vya siasa pia,” anaongeza.
Haki na amani
Katikati ya mjadala huo, Profesa Benson Bana ameshauri kuzingatiwa misingi mitatu ya kuunganisha jamii ambayo ni amani, haki na uhuru.
“Kwangu mimi na usomi wangu na uzoefu wangu, amani, haki na uhuru ni mafiga matatu ambayo huwezi kuyatenganisha. Hauwezi kupata amani pasipo haki, hauwezi kupata uhuru pasipo amani, hivyo wanasiasa wetu wasiogope kutamka mambo haya kwa pamoja badala ya kuchukua moja tu,” amesema.
Profesa Bana anasema maridhiano ya kitaifa baada ya ripoti hiyo yanapaswa kuzingatia zaidi makundi ya vyama vya siasa yenye mitazamo tofauti, akisisitiza kuwa msingi usiwe kwenye uharaka, bali ukweli na uimara wa maridhiano hayo.
“Tunao wazee wa busara, viongozi wa vyama vya siasa vyenye ushawishi, wanataaluma, wadau mbalimbali kuanzia gazi za chini hadi Taifa tuzungumze lugha moja. Yeyote anayekisiwa kuwa alihusika au kuna mahali alikengeuka, kwenye Tume hiyo aungame twende kwenye maridhiano twende kwenye Katiba mpya tukiwa wamoja,” amesema.