Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump, ameondolewa  ghafla kutoka jukwaani baada ya kutokea milio ya risasi na kuvuruga hafla ya White House Correspondents’ Dinner iliyokuwa ikiendelea jijini Washington, DC usiku wa kuamkia leo Jumapili, Aprili 26, 2026.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka mamlaka za usalama, tukio hilo lilitokea baada ya mshukiwa huyo aliyekuwa na silaha  kujaribu kuvamia eneo la ukaguzi linalolindwa na maofisa usalama.

Katika purukushani hizo, risasi zilifyatuliwa na kusababisha taharuki miongoni mwa wageni, waandishi wa habari na viongozi wa serikali waliokuwepo.

Rais Trump, ambaye alikuwa akizungumza jukwaani muda mfupi kabla ya tukio hilo, aliondolewa haraka na walinzi wake pamoja na mkewe Melania Trump, huku maofisa wengine waandamizi wa serikali wakiwemo wajumbe wa Baraza la Mawaziri wakihakikishiwa usalama.

Picha na Mtandao.

Baadaye, Trump aliwahakikishia wananchi kuwa yeye na timu yake wako salama.

“Tuliondolewa haraka sana bila muda wa kufikiria. Mwanzoni nilidhani ni kelele ya vitu kuanguka, lakini baadaye nikajua kulikuwa na hatari,” amesema Trump alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo.

Mamlaka zimethibitisha kuwa mshukiwa huyo, mwenye umri wa miaka 31 kutoka jimbo la California, amekamatwa na anashikiliwa na vyombo vya dola.

Taarifa zinaeleza mtuhumiwa huyo atafunguliwa mashtaka mawili likiwemo kutumia silaha kwa kufanya uhalifu na kuwashambulia maofisa wa serikali kwa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa awali, mshukiwa huyo alifanikiwa kufyatua angalau risasi moja kabla ya kudhibitiwa. Inaelezwa pia alikuwa na silaha zaidi ya moja wakati akijaribu kuvuka eneo la ukaguzi wa usalama.

Katika tukio hilo, wakala mmoja wa Secret Service alipigwa risasi lakini alinusurika kutokana na kuvaa vifaa maalumu vya kujikinga. Amepelekwa hospitali kwa matibabu na hali yake inaelezwa kuwa imara. Hakuna majeruhi wengine walioripotiwa.

Meya wa Washington, DC, Muriel Bowser amesema hakuna taarifa zozote zinazoonyesha kulikuwa na washirika wengine katika tukio hilo, huku akisisitiza uchunguzi unaendelea kubaini lengo la mshukiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Federal Bureau of Investigation (FBI), Kash Patelbametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa yoyote inayoweza kusaidia uchunguzi.

Amesema wataalamu wanaendelea kuchunguza silaha zilizokutwa eneo la tukio pamoja na kuhoji mashuhuda mbalimbali.

Mwandishi wa CNN, Wolf Blitzer, ambaye alikuwa nje ya ukumbi wakati tukio linatokea, amesema alishuhudia mshambuliaji akifyatua risasi umbali mfupi kutoka aliposimama, hali iliyosababisha watu wengi kukimbia na kujificha.

Hafla ya White House Correspondents’ Dinner ni tukio la kila mwaka linalowakutanisha viongozi wa serikali, waandishi wa habari na watu mashuhuri kwa ajili ya kuimarisha mahusiano kati ya vyombo vya habari na serikali ya Marekani.

Akizungumzia tukio hilo, Trump amesema licha ya hatari hiyo, anaamini tukio hilo limewaunganisha Wamarekani na kusisitiza kuwa hatua zaidi za usalama zitaimarishwa katika hafla zijazo.

“Urais ni kazi yenye hatari, lakini hatuwezi kuishi kwa hofu,” amesema.

Wakati uchunguzi ukiendelea, mamlaka zimeimarisha ulinzi katika maeneo muhimu jijini Washington, huku zikiahidi kutoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana.

Tukio hilo limeibua tena mjadala kuhusu usalama wa viongozi wa umma na ongezeko la matukio ya vurugu za kutumia silaha nchini Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *