Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amethibitisha tena uungaji mkono wa Pyongyang kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, akiahidi kuisaidia Moscow kupata ushindi katika “vita yake takatifu,” vyombo vya habari vya serikali vimeripoti leo Jumatatu.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Na: RFI na mashirika mengine

Matangazo ya kibiashara

Taarifa hii inakuja huku mfululizo wa maafisa wa ngazi za juu wa Urusi wakizuru Pyongyang katika siku za hivi karibuni, akiwemo Waziri wa Ulinzi wa Urusi Andrei Belousov, ambaye alikutana na Kim Jong Un siku ya Jumapili.

Korea Kaskazini “itaunga mkono kikamilifu sera ya Shirikisho la Urusi inayolenga kutetea uhuru wa kitaifa, uadilifu wa eneo, na maslahi ya usalama,” Kim Jong Un amemwambia waziri wa Urusi, kulingana na shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA.

Kiongozi huyo ameelezea “imani yake kwamba jeshi la Urusi na raia wake bila shaka watapata ushindi katika vita hivi vitakatifu na vya haki.”

Pande hizo mbili zimeonyesha kuwa zimejadili kuimarisha uhusiano wa kijeshi, huku Andrei Belousov akibainisha kuwa Moscow iko tayari kusaini mpango wa ushirikiano unaohusu kipindi cha mwaka 2027-2031.

Kim Jong Un, Andrei Belousov, na Spika wa Duma ya Serikali ya Urusi, Vyacheslav Volodin, pia wamehudhuria uzinduzi wa kumbukumbu ya kuwaenzi wanajeshi wa Korea Kaskazini waliouawa nchini Ukraine.

Korea Kaskazini imetuma maelfu ya wanajeshi, pamoja na makombora na risasi, kuiunga mkono Urusi katika vita vyake dhidi ya Ukraine.

Korea Kusini inakadiria kwamba takriban wanajeshi 2,000 wa Korea Kaskazini wameuawa katika mzozo huu.

Kwa kubadilishana, kulingana na wataalamu, Korea Kaskazini inapokea msaada wa kifedha, teknolojia ya kijeshi, pamoja na chakula na rasilimali za nishati kutoka Urusi, na kuiruhusu Pyongyang kuepuka vikwazo vizito vya kimataifa vilivyowekwa kwenye programu zake za nyuklia zilizopigwa marufuku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *