Mashambulizi mapya kati ya Israeli na Kundi la Hezbollah ambayo yamesababisha vifo vya watu 18 Kusini mwa Lebanon, yamekwamisha kuanza kwa mazungumzo ya kutekeleza mkataba wa kumaliza vita kati ya Marekani na Iran, yaliyokuwa yafanyike siku ya Ijumaa nchini Uswizi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ripoti za hivi karibuni zinasema, Israeli na Hezbollah, zimekubaliana kurejelea tena mkataba wa kusitisha vita, kwa mujibu wa afisa wa juu wa Marekani aliyenukuliwa na Shirika la Habari la Uingereza Reuters.
Mapema siku ya Ijumaa, jeshi la Israeli lilisema, limeshambulia ngome 80 za Hezbollah nchini Lebanon na kuwauwa wapiganaji kadhaa, wakiwemo wanajeshi wanne wa Israeli.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema jeshi la Israeli litaendelea kuwa nchini Lebanon kwa muda mrefu na Hezbollah watalipia gharama kubwa kwa kuishambulia nchi yake.
Mapigano haya mapya yamesababisha kukwama kwa mazungumzo kati ya mjumbe wa Iran Mohammad Bagher Ghalibaf na Makamu wa rais wa Marekani JD Vance nchini Usiwzi.
Ikulu ya White House imetangaza kuwa mazungumzo hayo yameahirishwa na Vance hatokwenda nchini Uswizi kama ilivyopangwa.
Mazungumzo hayo yalikuwa yaanze leo Ijumaa na kuendelea kwa miezi miwili kujadili maswala tata, likiwemo lile la mradi wa nyuklia wa Iran, baada ya mkataba wa kumaliza vita kutiwa saini kati ya Marekani na Iran wiki hii.