MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize, ametajwa miongoni mwa wanamichezo watatu bora walioteuliwa kuwania Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2025 inayotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), akitarajiwa kukutana na upinzani mkali kutoka kwa mwanariadha Alphonce Simbu na bondia Salmin Khamis.

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Mei 9, 2026 katika ukumbi wa Super Dome, uliopo Masaki, Dar es Salaam, ambapo wanamichezo bora nchini watatambuliwa kwa mafanikio yao ya mwaka uliopita.

Mzize amepata uteuzi huo kufuatia kufanya vizuri mwaka 2025 akiwa na Yanga, ambapo alionyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao na kuwa miongoni mwa washambuliaji chipukizi wanaovutia zaidi nchini huku pia akishinda Tuzo ya Bao Bora kutoka CAF.

MZI 01

Hata hivyo, anakutana na ushindani mkali kutoka kwa Simbu, ambaye ni miongoni mwa wanariadha bora wa Tanzania kimataifa kutokana na mafanikio yake katika mashindano ya marathon, pamoja na Khamis, ambaye ameendelea kung’ara katika ngumi za kulipwa na kuitangaza vyema Tanzania kimataifa.

Katika upande wa wanawake, Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Kike itawashirikisha Stumai Abdallah (mpira wa miguu), Magdalena Shauri (riadha) na Merciana Kizenge (mpira wa kikapu), wote wakiwa wamefanya vizuri katika michezo yao.

MZI 02

Kwa upande wa timu, tuzo ya Timu Bora ya Taifa (wanaume) itawashirikisha Taifa Stars, timu ya kriketi ya U-19, na timu ya ngumi ya ridhaa ya Tanzania. Kwa wanawake, walioteuliwa ni Twiga Stars, timu ya taifa ya mpira wa kikapu na timu ya tenisi ya viti mwendo.

Katika waamuzi, kipengele cha mwamuzi bora (wanaume) kinawajumuisha Ahmed Arajiga (mpira wa miguu), Shaaban Mahobonya (mpira wa kikapu) na Jeremia Keema (kuogelea). Kwa wanawake, walioteuliwa ni Tatu Malogo (mpira wa miguu) na Dariso Mwidadi (mpira wa kikapu).

MZI 03

Kwa upande wa makocha, katika wanawake wameteuliwa Esther Chabruma (mpira wa miguu) na Mariamu Kiwelo (mpira wa kikapu), huku kwa wanaume wakiwa Mohamed Mbwana (mpira wa kikapu), Anthony Mwingereza (riadha) na Samwel Kapungu (ngumi za ridhaa).

Vipaji chipukizi pia vimepewa nafasi, ambapo kwa wavulana walioteuliwa ni Luqman Mbalasalu (mpira wa miguu), Raphael Michael (mpira wa kikapu) na Raymond Francis (kriketi). Kwa wasichana, ni Esther Maseke (mpira wa miguu), Rose Katamboy (mpira wa kikapu), na Jenifer Kimaro (kriketi).

Tuzo hizo zinatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuhamasisha maendeleo ya michezo nchini Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *