Baada ya kutoonekana uwanjani kwa takribani miezi mitatu, hatimaye straika wa Mbeya City, Yacouba Songne amerejea na kuanza mazoezi mepesi akitumia takribani dakika 60 kujifua.
Yacouba raia wa Burkina Faso, alijiunga na Mbeya City kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu huu ambapo mara ya mwisho alionekana Februari 7, 2026 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya TRA United uliopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, na kupata majeraha ya goti.
Leo Mwanaspoti imemshuhudia staa huyo akijifua kivyake wakati wenzake wakiendelea na program chini ya Kocha Mkuu, Salum Mayanga kujiwinda na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa, utakaochezwa Aprili 30, 2026.
Wakati Yacouba akirejea, kipa wa timu hiyo, Beno Kakolanya ameendelea kukosekana huku ikielezwa kuwa bado ana matatizo ya kifamilia.
Ofisa Habari wa Mbeya City, Gwamaka Mwankota, amesema Yacouba alikuwa majeruhi na sasa amerejea, hivyo hatma ya kuonekana mchezoni itategemeana na uamuzi wa kocha Mayanga.
“Kuhusu Kakolanya bado ana matatizo ya kifamilia, Yacouba amerejea, hivyo hatma yake zaidi ipo kwa Kocha Mayanga kama ataona anafaa kutumika kuanzia mechi ijayo ya Mashujaa,” amesema Mwankota.
Wakati huo huo, Mwankota amethibitisha Jeremia Kisubi kutua kikosini humo kuwa Kocha wa Makipa kusaidiana na benchi la ufundi kwa mechi zilizobaki kabla ya kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2025-2026.