
Dodoma. Wizara ya Kilimo imetaja vipaumbele sita katika kutekeleza bajeti ya Sh1.1 trilioni kwa mwaka 2026/27, huku miradi ya Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) na ubora wa mbegu vikipewa kipaumbele.
Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuongeza tija na uzalishaji, kuongeza ajira zenye staha, na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pamoja na upatikanaji wa mitaji, masoko na mauzo nje ya nchi.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha maendeleo ya ushirika na kuimarisha matumizi ya mifumo ya Tehama katika uendelezaji wa sekta ya kilimo, na katika kufanikisha hilo, wizara imepanga kutekeleza mikakati 30.
Hata hivyo, bajeti ya 2026/27 ni pungufu kidogo ya bajeti ya mwaka 2025/26, ambayo ilikuwa Sh1.2 trilioni, ikiwa na vipaumbele sita na mikakati 27, huku miradi ya BBT ikiwa sehemu ya kipaumbele cha kwanza.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imebainisha utolewaji usioridhisha wa fedha za miradi ya maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge, jambo linaloathiri utekelezaji wa shughuli za wizara.
Mathalani, kati ya Sh16 bilioni zilizopitishwa kwa ajili ya miradi ya BBT, ni Sh6 bilioni pekee zimetolewa hadi Februari 2026. Fedha za maendeleo ni asilimia 55.39 pekee zilizotolewa.
Uelekeo wa 2026/27
Akiwasilisha bajeti yake kwa mwaka 2026/27, leo Aprili 28, 2026, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ameliambia Bunge wanafanya hayo ili kuimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora na miche, ikiwemo utoaji wa ruzuku ya mbolea, mbegu na viuatilifu.
Waziri Chongolo ametaja mikakati mingine kwenye bajeti hiyo kuwa ni usajili wa wakulima na urasimishaji wa shughuli za kilimo katika huduma za ugani, kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja na kupima afya ya udongo.
“Kwa kuzingatia changamoto ya upatikanaji wa ajira, hususan kwa vijana na wanawake, wizara imepanga kuwezesha uendelezaji wa programu ya BBT ngazi ya halmashauri, kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwa wakulima wadogo (BBT visima), na kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa vijana na wanawake (BBT mitaji),” amesema Chongolo.
Kwenye miradi ya BBT, Chongolo amesema watawezesha vijana na wanawake kuzalisha miche (BBT miche), kuongeza thamani ya mazao na kuwezesha vijana na wanawake kutoa huduma za ugani (BBT ugani).
Kuhusu uhifadhi wa chakula, amesema ili kuwezesha nchi kuendelea kujitosheleza katika usalama wa chakula na lishe, Serikali itaongeza msukumo kwa wakulima katika kilimo cha kisasa na kutoa elimu ya matumizi sahihi ili kufikia malengo ya kuhifadhi tani milioni 3 ifikapo 2027.
Akizungumzia eneo la ushirika, amesema kwa bajeti ijayo, wizara imepanga kutekeleza mikakati, ikiwemo kuimarisha maendeleo ya ushirika nchini, kuimarisha ukaguzi na usimamizi wa uendeshaji wa vyama vya ushirika, kuimarisha ushirika kwenye sekta mbalimbali na makundi maalum, na kuhamasisha vyama vya ushirika kujiendesha kibiashara.
Waziri huyo amesema kazi mojawapo katika kuimarisha mnyororo wa kilimo ni kuongeza tija na uzalishaji, lakini Serikali pia itaimarisha shughuli za utafiti wa kilimo, kwa kuwa ndiyo msingi wa ukuaji wa sekta ya kilimo unaowezesha ugunduzi na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo mbegu bora na matumizi sahihi ya udongo na maji.
Amesema wizara, kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), itakamilisha ugunduzi na kusajili aina 73 za mbegu bora za mazao ya kimkakati ya nafaka, jamii ya mikunde, biashara, mizizi, matunda na mafuta, kwa lengo la kuongeza aina mpya za mbegu zinazoendana na mahitaji ya soko.
“Kukamilika kwa tafiti hizo kutawezesha mapendekezo ya matumizi sahihi ya mbolea, na itakamilisha uchambuzi wa sampuli 34 za udongo zilizokusanywa kwa ajili ya utafiti wa afya ya udongo ili kubaini kiwango sahihi cha uwekaji wa mbolea ya kupandia na kukuzia,” amesema Chongolo.
Kuhusu mbegu, amesema wizara itaendelea uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora na miche, kwani mahitaji ya mbegu bora nchini kwa mwaka ni tani 127,650. Hivyo, kwa bajeti ya 2026/27, wizara kwa kushirikiana na sekta binafsi imepanga kuongeza upatikanaji wa mbegu bora kutoka tani 79,214.48 mwaka 2025/26 hadi tani 127,650.
Amesema wataongeza uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi kutoka tani 47,702.45 mwaka 2025/26 hadi tani 105,000 mwaka 2026/27, ambapo Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) itazalisha mbegu bora tani 27,219 kupitia kilimo cha mkataba kwa kampuni na wakulima kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 12,470.
“Msingi wa mapinduzi ya kilimo unaanza na mbegu bora, ambazo hubeba hatma ya mavuno yetu na ni kiini cha tija na usalama wa chakula kwa nchi kwa ujumla.
“Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wakulima kuhusu uwepo wa mbegu zisizo na ubora kutoka kwa wafanyabiashara wasio waaminifu,” amesema Waziri na kuongeza;
“Nitoe wito kwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanaouza mbegu zisizo na ubora kufahamu kuwa mkono wa sheria hautawaacha salama. Niwasihi wakulima wa nchi hii kuwa macho na kuhakikisha wananunua mbegu bora kutoka kwa mawakala waliosajiliwa,” amesema.
Kwenye suala la mbolea, amesema Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) itaanzisha kiwanda cha kutengeneza chokaa kwa ajili ya mazao chenye uwezo wa kuzalisha tani 250,000 hadi 500,000 kwa mwaka, huku ikiweka mkakati kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Serikali pia inakuja na mkakati wa uzalishaji wa sukari, ambapo Bodi ya Sukari Tanzania itaongeza uzalishaji wa zao la miwa kutoka tani 4,351,673.1 zilizozalisha sukari tani 410,979.04 mwaka 2025/26 hadi kufikia tani 5,500,000 za miwa zitakazozalisha sukari tani 550,000, lengo likiwa kufikia hatua ya kuwa na sukari toshelevu.
Miradi ya BBT
Waziri Chongolo amesema wanakuja na mkakati wa miradi hiyo kwa ngazi ya halmashauri 20, zilizotenga maeneo yasiyopungua ekari 200 katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Njombe, Mbeya, Iringa, Pwani, Mara, Katavi, Rukwa, Kagera na Geita.
Vilevile, wizara itawajengea uwezo vijana 2,000 watakaochaguliwa na halmashauri zao kuhusu kilimo biashara kupitia programu ya BBT kwenye vyuo na vituo vya mafunzo ya kilimo.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika, ameomba Serikali kuongeza matumizi ya vyanzo vya ndani vya mapato badala ya kutegemea fedha za nje ambazo zimekuwa hazipatikani kwa uhakika.
Amesema mradi wa BBT uliidhinishiwa Sh16 bilioni fedha za ndani, lakini hadi Februari 2026, fedha zilizopokelewa ni Sh6 bilioni sawa na asilimia 37.50 ya bajeti.
“Utolewaji huu wa fedha umeathiri utekelezaji wa miradi ya BBT na hivyo kupelekea kushindwa kufikia malengo ya kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo,” amesema Mwanyika.
Mwanyika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge, amesema kiasi cha fedha kilichopokelewa kwa miradi ya maendeleo ni asilimia 55.39 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili hiyo.
“Mtiririko huu wa fedha kwenye miradi ya maendeleo unaathiri utekelezaji wa majukumu ya wizara, hasa kwenye mradi wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo Tanzania na programu ya maendeleo ya kilimo, ambayo tayari ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake.
“Jambo hili linaathiri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichoahidi kuendelea kusimamia mapinduzi ya kilimo ili kuhakikisha kinakuwa na tija na kinatumia teknolojia ya kisasa,” amesema.
Kamati imeeleza kuwa kupungua kwa bajeti kunakinzana na makubaliano ya kimataifa ya kuongeza uwekezaji kwenye kilimo, hivyo imeitaka Serikali kuongeza bajeti ili kufikia lengo la kutenga angalau asilimia 10 ya bajeti ya taifa kwa sekta hiyo.