
Kiteto. Ekari tano tofauti zilizolimwa dawa za kulevya aina ya bangi katika mashamba ya mahindi kwenye kijiji cha Mbigili Kata ya Partimbo, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, zimetekelezwa kwa moto katika operesheni iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Remidius Mwema.
Mwema akishirikiana na baadhi ya wananchi wa eneo hilo jana Jumatatu, Aprili 27, 2026 waliteketeza kwa moto ekari tano tofauti za mashamba ya bangi zilizooteshwa kwenye mazao ya mahindi.
Mwema akiwa na kamati ya usalama ya wilaya hiyo akizungumza wakati wakiteketeza mashamba hayo kwenye Kijiji cha Mbigili, amesema mapambano ya dawa za kulevya ni suala endelevu kwani zinasababisha athari kubwa za kiafya na kijamii.
Ameeleza kuwa wamechoma moto baada ya kubaini dawa hizo za kulevya aina ya bangi zikiwa zimepandwa pamoja katika ekari tano tofauti za mashamba hayo ya mahindi.
Amesema ameagiza wamiliki wa mashamba hayo wakamatwe ili uchunguzi ufanyike na kubaini kuwa endapo wameyakodisha au wamelima wenyewe.
“Wamiliki wa mashamba haya wanajulikana sasa hatujaelewa kama wamelima wenyewe au walikodisha wakalima wengine, hivyo wakamatwe ili uchunguzi ufanyike,” amesema Mwema.
Amesema operesheni hiyo ni maalumu kuhakikisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafanikiwa katika eneo hilo kutokana na ushirikiano wa jamii na askari.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbigili Omari Ngoda amesema shughuli hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, itawapa hofu na kukomesha kilimo hicho kwa wahusika.
Ngoda amesema shughuli hiyo itakuwa endelevu kwani wataendelea na ukaguzi wa mashamba na wakibaini wanaendelea kuchoma moto.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mbigili, wamepongeza jitihada za serikali katika kuteketeza kwa moto dawa hizo za kulevya kwani zilikuwa zinaathiri jamii wakiwemo vijana wao ambao ni nguvu kazi ya Taifa.
Mmoja kati ya wakazi hao Asia Salim amesema kitendo cha dawa hizo za kulevya aina ya bangi kuchomwa moto kimewapa faraja mno wananchi wa eneo la Mbigili.
“Tamaa yetu ya kuona vijana wetu wanaondokana na matumizi ya dawa za kulevya na kujishughulisha na kazi za mikono yao kuliko kuvuta bangi,” amesema Asia.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mohamed Zubeir ameeleza kuwa hatua hiyo ni nzuri kwani uteketezaji wa moto kwa dawa hizo za kulevya utakomesha ukuaji wake katika eneo hilo.
“Serikali inapiga vita dawa za kulevya na jamii inapaswa kuungana na viongozi katika kupiga vita matukio ya matumizi ya bangi, tumefurahi mno kitendo hiki cha kuteketeza bangi,” amesema Zubeir.