
Tabora. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kumtapeli zaidi ya Sh40 milioni mjane Fatuma Nassoro mkazi wa Kaliua mkoani Tabora.
Akizungumzia tukio hilo leo Aprili 28, 2026 Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amesema mbinu waliyoitumia watu hao ni kujifanya wao ni mawakala na wanasajili ‘Lipa namba’ hivyo wakaanza kazi hiyo na wakadai namba yake ya siri.
“Hawa watu wamejifanya ni mawakala wamemkuta huyu mama dukani kwake, anauza vitambaa Kaliua mjini, wakamuambia wana huduma ya lipa namba,mama akaona ni bora ili arahisishe huduma yake kumbe hakujua kama ni matapeli,” amesema Chacha.
Amesema watu hao wamemuambia mjane huyo kwamba ili huduma ya Lipa namba iweze kufanya kazi lazima iunganishwe na mfumo wa benki, hivyo wakamtaka aingize namba ya siri na kwamba baadaye huduma itakuwa tayari, wakambadilishia laini yake ya simu bila yeye kujua na wakaondoka.
“Wakaondoka pale, huyu mama alipotaka kufanya mawasiliano yake ya kawaida, anakashangaa simu hazitoki na baada ya kuhakiki akagundua line iliyopo kwenye simu siyo yake isipokuwa alikuta ujumbe mfupi kwenye simu kwamba line hiyo imetoa Sh900,000 ndipo kugundua kuwa ametapeliwa,” ameeleza.
Baada ya mwanamke huyo kuamua kwenda benki kuhakiki fedha zake hakukuta akiba aliyokuwa ameweka takribani Sh40 milioni badala yake akakuta Sh6,000 pekee.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao ameeleza kwamba watuhumiwa hao baadhi ya fedha hizo wamenunua gari lakini zingine wamekeshea bar wakinywa, huku mtuhumiwa mmoja akiomb arudishe fedha kidogo kidogo kwa kutoa Sh10 milioni kwa wiki.
“Wanatufanya kuwa sisi hatuna akili, kwa sababu mtu amefanya utapeli halafu anasema atazirudisha kwani kila wiki atatoa Sh10 milioni, sasa anashawishi sisi tumuachie ili akatapeli wengine aje alipe fedha za mama huyu,” amesema.
Kamanda Abwao amesema watuhumiwa hao wamekamatiwa Babati mkoani Manyara baada ya kutoka Kaliua kumtapeli mjane huyo,
“Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hii ili kubaini mtandao mzima lakini huenda kukawa na matukio mengine yaliyotekelezwa na watu hawa,” amesema.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora kuacha tabia ya kutoa namba ya siri kwa watu wasiowajua kwani hatua hiyo inahatarisha usalama wa fedha zao.
Kwa Upande wake mjane huyo Fatuma amesema akiwa dukani walifika watu hao waliodai kuwa ni watoa huduma kutoka kampuni moja ya simu (jina limehifadhiwa)wakimpa huduma ya lipa namba kisha baadaye wakamuibia.
“Nilipogundua nimetapeliwa nikaenda kwa meneja wa benki aniangalizie salio, ndipo akaona fedha zangu zimetolewa na akanishauri niende nikatoe taarifa polisi,” ameeleza.