
Dar es Salaam. Daktari wa Kituo cha Afya Kinyerezi, Matayo Petrol ameieleza mahakama kuwa baada ya kumfanyia vipimo mshtakiwa Dominic Mushi, vilionyesha kuwa alikuwa amekunywa dawa nyingi hali ambayo ingesababisha kupoteza maisha.
Pia mdomoni kwake, Mushi alikutwa akiwa na mabaki ya chengachenga nyeupe zinazodaiwa kuwa ni dawa.
Dk Petrol ametoa ushahidi wake leo Jumanne, Aprili 28, 2026 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisuti, katika kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Gongolamboto Dominic Mushi
Mushi anakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mkewe Diana, tukio analodaiwa kulitenda Oktoba 14, 2024 eneo la Kinyerezi Kichangani, lililopo wilaya ya Ilala.
Diana ambaye alikuwa mfanyakazi wa benki ya NMB tawi la Airport, anadaiwa kuuawa na mumewe na mwili wake ulikutwa kitandani ukitoka damu eneo la puani, masikioni na mdomoni.
Mshtakiwa huyo anadaiwa katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa Kituo cha Polisi Stakishari, alidai kuwa kelele za kuomba msaada alizokuwa akizitoa mke wake siku hiyo usiku ilikuwa ni ndoto kwani mke wake alikuwa anaota.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili wa Serikali, Hakme Pembe, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube aliyepewa Mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo ya mauji, alidai Oktoba 14, 2024 mchana alipokea mgonjwa aitwaye Dominic Mushi (34), aliletwa na polisi, ndugu zake wakiwa na fomu namba tatu ya polisi (Pf3) ya tuhuma za mauaji.
Dk Petrol alidai mgonjwa huyo alikuwa akitokwa na mapovu mdomoni na alipelekwa kituo hapo kwa ajili ya matibabu akiwa amepoteza fahamu.
“Nilimfanyia vipimo vya awali vya presha, ugonjwa wa moyo na kupima oksijeni katika damu ambapo vipimo vyote vilikuwa sawa na kawaida.Nilielekeza muuguzi ampeleke katika chumba cha mapumziko mgonjwa huyo kwa sababu alikuwa hajitambui”amesema Dk Petro.
Pia alimfanyia vipimo mgonjwa kwa kumtazama chini hadi juu ambapo alibaini chengachenga nyeupe ndani ya mdomo wake.
“Nilipohoji waliomleta, walisema pembeni ya mgonjwa walipomchukua kulikuwa na kopo la dawa ambazo hawakuzijua kwa majina” amedai shahidi
Alidai kutokana na hali hiyo, aliamua kumpima mifumo ya fahamu ya mwili kwa sababu alipoteza fahamu na kwa wakati huo mgonjwa alikuwa hajitambui.
“Niliagizia vipimo vya maabara kwa kupima malaria, wingi wa damu na sukari, majibu ya vipimo vilikuwa sawa.Hata hivyo, matokeo ya vipimo vilikuwa sawa na kwa historia ya vipimo nilibaini mgonjwa alikunywa dawa nyingi hali ambayo ingesababisha kupoteza maisha” amedai.
Baada ya kugundua hilo, walimfanyia huduma ya kwanza kwa kumtundikia dripu, kumpa dawa ili aweze kurudi katika hali ya kawaida.
Shahidi huyo alidai baada ya kumpatia huduma ya kwanza mgonjwa huyo, alijaza PF3 na kisha alitoa rufaa ya Mushi kupeleka hospitali ya Amana kwa ajili ya uchunguzi zaidi.