Manchester, England. Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes ameendelea kuonyesha kiwango cha juu kilichoisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brentford katika mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa Old Trafford.

Ushindi huo umeisukuma United hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi huku ikizidisha matumaini ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, wakati vijana wa kocha Michael Carrick wakihitaji pointi chache tu kuthibitisha ndoto hiyo.

United ilianza vyema baada ya Casemiro kufunga bao la kwanza kwa kichwa, akitumia pasi iliyotengenezwa na Haary Maguire kufuatia mpira wa kona uliochongwa na Fernandes.

Katika kipindi chote cha mchezo, Brentford walionesha upinzani wa hali ya juu wakitengeneza nafasi kadhaa za kusawazisha, lakini uimara wa safu ya ulinzi ya United uliifanya timu hiyo kuendelea kuongoza.

Bao la pili la United lilifungwa na Benjamin Sesko baada ya kupenyezewa pasi kutoka kwa Fernandes, ambaye sasa anakaribia kuvunja rekodi ya kupiga pasi nyingi za mabao katika msimu mmoja wa Ligi Kuu England.

Hadi sasa kiungo huyo wa Ureno amehusika katika mabao 140 akifunga 70 na kutoa pasi za mabao 70, akiwa ndiye mchezaji pekee wa United ambaye amehusika katika mabao mengi EPL.

Licha ya Brentford kupata bao la kufutia machozi mwishoni mwa mchezo, haikutosha kuzuia ushindi wa United ambao unaonekana kuwa tiketi muhimu kuelekea katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Ushindi huo pia umeibua mjadala kuhusu mustakabali wa Fernandes, huku ikielezwa kuwa uongozi wa United uko mbioni kumsainisha mkataba mpya kiungo huyo.

Pamoja na kuondoka kwa baadhi ya nyota wakubwa, Fernandes ameendelea kuwa mhimili muhimu wa mafanikio ya United msimu huu, jambo linalofanya mchezaji huyo kupewa kipaumbele katika mipango ya baadaye.

Kwa upande mwingine, kiungo mkongwe Casemiro ameendelea kuonyesha ubora wake licha ya umri wake, ingawa inaelezwa kuwa huenda akaondoka mwishoni mwa msimu kutokana na sera za kupunguza matumizi zilizoanzishwa na mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Sir Jim Ratcliffe.

Kwa sasa, macho yote yako kwa Carrick ambaye amezidi kuthibitisha makali yake na huenda kocha huyo akakabidhiwa mikoba ya kudumu kutokana na mwendelezo wa matokeo chanya anayopata Klabuni hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *