
Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa sasa unaokwenda kasi, kuna swali moja ambalo limebaki kuwa mwiba kwa vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu: “Nitapata wapi kazi?”
Hata hivyo, kabla ya kuelekeza kidole cha lawama kwa Serikali au soko la ajira lililosinyaa, ni vyema tujitazame sisi wenyewe kama wazazi.
Ukweli mchungu ni kwamba, malezi yetu na mifumo ya fikra tunayowarithisha watoto wetu tangu wakiwa wadogo, ndiyo chimbuko la tatizo la ukosefu wa ajira linalowatafuna leo.
Tumebaki tukikariri mbinu za karne ya 20 kupambana na changamoto za karne ya 21, jambo ambalo ni sawa na kujaribu kufungua mlango wa kidijitali kwa kutumia ufunguo wa chuma uliopata kutu.
Tukirudi nyuma kidogo, miaka ya mwanzo baada ya uhuru na miongo iliyofuata, mfumo wa elimu ulikuwa na lengo moja kuu la kuziba mapengo ya watumishi wa umma walioondoka. Wakati huo, Taifa lilikuwa na watu wachache na mahitaji makubwa ya wataalamu wa kujenga nchi.
Mzazi alipomwambia mtoto “soma kwa bidii ili upate kazi nzuri,” alikuwa anasema ukweli wa wakati huo.
Kazi zilikuwa zinamsubiri mhitimu kabla hata hajashika cheti chake mkononi. Hata hivyo, mazingira hayo yamezikwa na wakati. Leo hii, idadi ya watu imeongezeka mara dufu, ushindani ni mkali, na teknolojia imechukua nafasi ya mikono ya watu.
Ni kosa la jinai kisaikolojia kuendelea kumlisha kijana wa leo matumaini yale yale ya mwaka 1970, tukijua fika kuwa mnyororo wa ajira rasmi umekatika.
‘Soma upate kazi’ na shimo la kukata tamaa
Mtazamo wa mzazi wa leo bado umeganda kwenye dhana kuwa mafanikio yanakuja tu kupitia mshahara wa mwisho wa mwezi.
Tunawaaminisha watoto wetu kuwa shule ni kiwanda cha kuzalisha watumishi, badala ya kuwa kituo cha kukuza maarifa na ubunifu.
Mtoto anasoma miaka zaidi ya 20 akiamini kuwa kuna ofisi yenye kiyoyozi inamsubiri. Anapohitimu na kukutana na ukuta wa ukosefu wa ajira, anachanganyikiwa na kuanza kujiona kuwa amefeli maisha.
Hapa ndipo tunapozalisha jeshi la vijana wenye vyeti lakini wasio na ujuzi wa kupambana na mazingira halisi ya uchumi.
Wazazi tunashindwa kuwaambia watoto wetu ukweli mapema kabisa; kuwa ajira serikalini au kwenye kampuni binafsi sasa hivi ni bahati nasibu, na si haki ya kila mhitimu.
Inasikitisha kuona mzazi ambaye ni mjasiriamali aliyefanikiwa, anayemiliki duka kubwa Kariakoo au anayefuga mifugo mingi shambani kwake, hamshirikishi mtoto wake kwenye shughuli hizo.
Tunawalea watoto wetu kama “mayai” tukiamini kuwa kuwagusa na jembe au kuwaingiza sokoni ni kuwatesa. Mzazi anafanya biashara usiku na mchana ili amlipie mwanawe ada ya chuo kikuu, lakini hamfundishi jinsi ya kupiga hesabu za faida na hasara au jinsi ya kunadi bidhaa.
Matokeo yake, mtoto anamaliza shahada ya biashara lakini hawezi hata kusimamia duka la familia. Tunawasubirisha waajiriwe, huku tukiwa tumewazunguka na fursa za kujiajiri ambazo sisi wenyewe tunazitumia kutunza familia zetu.
Huu ni upofu wa kimkakati unaowaacha vijana wetu wakiwa tegemezi hata wakiwa na umri wa miaka thelathini.
Mapinduzi ya fikra
Wakati umefika kwa wazazi kubadilika na kuanza kuwa chachu ya mabadiliko. Badala ya kumwambia mtoto asome ili aajiriwe, mweleze asome ili apate maarifa yatakayomsaidia kutatua matatizo ya jamii na kujitengenezea kipato.
Nyumbani lazima pawe shule ya kwanza ya ujasiriamali. Ikiwa unafuga kuku, mpe mtoto jukumu la kusimamia kundi moja na amueleze namna ya kutafuta masoko.
Ikiwa una biashara ndogo, mfundishe nidhamu ya fedha na huduma kwa wateja tangu akiwa shule ya msingi.
Hii haimzuii mtoto kufanya vizuri kimasomo, bali inampa “Plan B” imara pindi soko la ajira rasmi litakapomgeuzia mgongo.
Lazima tuwaaminishe kuwa kufanya kazi kwa mikono au kuanzisha mradi mdogo si ishara ya kufeli, bali ni ushujaa wa kupambana na hali halisi.
Ili kuwasaidia watoto wetu kuwa na ajira zao wenyewe, tunahitaji mikakati madhubuti ya malezi. Kwanza, wazazi tunapaswa kugundua na kulea vipaji vya watoto wetu mapema.
Ikiwa mtoto anaonyesha uwezo wa ufundi, sanaa, au teknolojia, tusiwashurutishe kufuata mkondo wa masomo ya “hadhi” tunayotaka sisi.
Pili, tuwawezeshe watoto wetu kuanza miradi midogo wakiwa bado wapo masomoni. Hata kama ni biashara ya mtandaoni au kutoa huduma fulani kwa jamii, hiyo inawajengea ujasiri na uzoefu ambao hautolewi darasani.
Tatu, lazima tubadilishe lugha yetu; badala ya kuuliza “utafanya kazi wapi?”, tuanze kuuliza “utatengeneza kazi gani?”. Kwa kufanya hivi, tutakuwa tumewaandalia urithi wa kudumu ambao hautategemea saini ya mwajiri yeyote, bali utategemea nguvu ya akili na mikono yao wenyewe.