Dar es Salaam. Lori lililokuwa limebeba makontena limepinduka katika barabara ya Kilwa eneo la Mbagala Mission na kusababisha msongamano mkubwa wa magari uliosambaa hadi kwenye barabara ya mwendokasi, huku watumiaji wa barabara wakikumbwa na adha ya usafiri kwa saa kadhaa.
Ajali hiyo imetokea asubuhi ya leo Jumanne, Aprili 28, 2026 katika barabara hiyo muhimu inayounganisha jiji na maeneo ya Mbagala, ambapo lori hilo lilipoteza mwelekeo na kuanguka katikati ya barabara, hali iliyoziba njia na kusababisha magari kushindwa kupita.
Kutokana na tukio hilo, msongamano wa magari uliongezeka na kuathiri hata njia ya mabasi yaendayo haraka (mwendokasi), jambo lililosababisha foleni na kuacha abiria wakisubiri kwa muda mrefu.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema hali ilikuwa ngumu baada ya lori hilo kuanguka, huku baadhi ya madereva wakilazimika kusimamisha magari yao kwa muda mrefu na wengine kujaribu kupenya pembezoni mwa barabara bila mafanikio.
Lori lenye makontena likiwa limepinduka na kuziba barabara eneo la Mbagala Mission. Ajali hii imesabababisha msongamano na adha kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa.
“Nilikuwa natoka Mbagala kuelekea katikati ya jiji, ghafla tukakutana na foleni kubwa. Tulipofika mbele ndipo tukakuta lori limeanguka na limeziba barabara yote,” amesema dereva wa daladala, Juma Hamisi.
Shuhuda mwingine, ambaye ni mfanyabiashara wa eneo hilo, Asha Mhando amesema tukio hilo liliathiri pia shughuli za biashara kwa kuwa wateja wengi walishindwa kufika kwa wakati.
“Hii barabara ikisimama tu, kila kitu kinakwama. Watu hawafiki kazini, biashara zinadorora. Leo hali ilikuwa mbaya zaidi kwa sababu hata mwendokasi ulikuwa umejaa,” amesema Asha.
Kwa upande wake, dereva wa teksi mtandao, Kelvin Mrema amesema alilazimika kusitisha safari zake kwa muda kutokana na msongamano huo.
“Nimekaa kwenye foleni zaidi ya saa moja bila kusogea. Abiria wengine waliamua kushuka na kuendelea kwa miguu. Hii hali inaleta hasara kubwa kwetu madereva,” amesema.
Katika juhudi za kupunguza athari za tukio hilo, askari wa usalama barabarani walionekana wakisimamia na kuelekeza magari wakihakikisha angalau baadhi ya magari yanapata nafasi ya kupita licha ya lori hilo kuziba barabara.
Lori lenye makontena likiwa limepinduka na kuziba barabara eneo la Mbagala Mission. Ajali hii imesabababisha msongamano na adha kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa.
Mashuhuda wamesema askari hao walifanya kazi kwa bidii kubwa chini ya shinikizo la msongamano, wakibadilisha mwelekeo wa magari mara kwa mara na kuwasihi madereva kufuata maelekezo ili kuepusha kuongeza msongamano.
“Askari walijitahidi sana, walikuwa wanapanga magari yapishane kidogo kidogo. Kama si wao hali ingekuwa mbaya zaidi,” amesema mmoja wa abiria.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameitaka Serikali na mamlaka za usafiri kuchukua hatua za kudhibiti ajali za mara kwa mara zinazohusisha malori ya makontena katika Barabara ya Kilwa, wakieleza zimekuwa zikisababisha usumbufu mkubwa na kuhatarisha maisha ya watu.
Lori lenye makontena likiwa limepinduka na kuziba barabara eneo la Mbagala Mission. Ajali hii imesabababisha msongamano na adha kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa.
Wamesema kuna haja ya kuweka utaratibu madhubuti wa usimamizi wa magari makubwa, ikiwemo ukaguzi wa mara kwa mara na udhibiti wa mwendokasi, ili kupunguza hatari ya ajali kama hizo kujirudia katika eneo hilo lenye msongamano wa magari.