Kuna mama mmoja, kabila hatutaji. Hawa jamaa wanaosifika kwa kuwachuna wenzao na kujenga kwao aliolewa na jamaa ambaye japo hakuonyesha, aliwajua vilivyo.

Kwa uzwazwa aliona ni ujanja, alijiona kapata asijue atapatikana baada ya kupata kwa muda ili apatwe. Badala ya kufunga ndoa ili kujenga familia yake, aliigeuza kitega uchumi kwa ajili ya familia yake na ndugu zake, asijue yakimkuta hiyo familia na ndugu hawataumia kama yeye.

Ni ujuha na upofu kiasi gani? Wenye ujuha na uzwazwa huu, hii makala ni yenu. Mtajifunza kitu. Kila siku, baba au mama mkwe alitaka hiki na kile. Mara kaka amefukuzwa shule. Hivyo, anahitaji karo arejee shuleni.

Mara dada kafanyiwa operesheni. Inahitajika pesa ya kulipia matibabu. Mara babu au bibi kateguka mguu. Anahitaji kwenda kuangaliwa. Ni pesa pande zote. Ajabu ya maajabu, wakati yeye akidai hili na lile, hakujiuliza. Hakuna hata siku moja mumewe aliwahi kuleta hoja kama hizo kwa upande wa familia yake.

Kunogesha stori, huyu juha hakuwa wala mrembo. Pia, aliolewa akiwa kwenye umri wa jioni kutokana na sura na tabia yake mbaya licha ya ujuha na uroho na roho mbaya.

Jamaa alifanya kila kitu makusudi. Japo alidhani kuwa buzi au fala, hakuwa. Alifanya mkusudi ili aweze kujua kama alikuwa amepata mke au mchunaji.

Baada ya kujiridhisha kuwa mle hamkuwa na kitu, aliweka mtego na kuachana na kahaba huyu. Alinaswa na mtego wake mwenyewe. Baada ya kudai kuwa babu yake alikuwa amelezwa kutokana na kuteguka mguu, mume alikuja na kumstukiza.

Bila hili wala lile, alirejea nyumbani akiwa ameishakamilisha mipango yote ya kwenda ‘kumuona mgonjwa.’ Mama alijitahidi kukataa safari isifanyike. Mumewe alimwambia kwa vile alikuwa si mgeni kijijini kwao, angeenda peke yake kwenda kumuona babu yao.

Kwa ujinga, baada ya kumpa taarifa hii iliyomstua na kumtikisa, ilipigwa simu kutoka kwa mama yake akisema babu alikuwa amerejeshwa nyumbani baada ya kugoma kulala hospital.

Kwa ujuha na uzwazwa wao, hawa wezi walidhani hii ingemzuia mkwe kwenda kumuona babu yake. Jamaa alishikilia msimamo wake. Mama hakuwa na la kufanya bali kukubali.

Kulipokucha, walifunga safari kwenda kumuona babu. Walimkuta akiwa amefungwa bandeji mguuni. Wajukuu walimtakia kila la heri apone haraka.

Hili, kwa muda liliwafanya wezi hawa wadhani walikuwa wameshinda. Hawakujua kuwa jamaa alikuwa amejiandaa kisaikolojia.

Wakiwa wanajibaraguza kumwambia uongo, mkwe alipiga simu kwa mdogo wake ambaye alikuwa daktari wa mifupa akijifanya hajui kitu kutaka amsaidie namna ya kumsadia babu yao.

Wezi husika walishikwa na butwaa wasijue la kufanya. Walidhani jamaa alikuwa akifanya kila kitu kutokana na upendo. Hawakujua alikuwa anataka kuwakaanga kwa mafuta yao. Aliweka simu kwenye kipaza sauti na kuongea na mdogo wake.

Alimuomba mdogo wake awasaidie. Bahati nzuri, mdogo wake alisema kuwa alikuwa na daktari wa mifupa waliyesoma pamoja pale kwenye hospitali iliyodaiwa alikuwa amepelekwa babu yao.

Moja kwa moja, mdogo mtu alimpigia huyo daktari na kuomba apewe namba ya mgonjwa. Jamaa aliwageukia hawa wachunaji na kuwataka wampe namba. Hawakutegemea. Waliangaliana na kuanza kutafuta visingizio.

Jamaa aliwapa muda. Alimshukuru mdogo wake na kukata simu akimuahidi kuwa alipokuwa amefikia, alikuwa ametoa msaada mkubwa kwao. Aliwageukia mkewe na wakwe zake na kuomba namba.

Hawakuwa nayo. Walijitetea kuwa babu alikuwa ameipoteza. Jamaa aliamua kuwaumbua zaidi. Alisema kwa vile alikuwa na simu aliyokuwa amepewa na mdogo wake, angempigia yule daktari wa mifupa afuatilie hospitalini kwake.

Walikiri na kuomba msaada. Jamaa aliwasamehe kwa kumuacha binti yao mbele yao akiahidi angemruhusu aende kuchukua vitu vyake na kuondoka milele.

Je, wapo wangapi kama hawa tena mazwazwa wanaojiona hata kujivuna kuwa wanachuna mabuzi wakati wasijue mabuzi mengine si mabuzi bali yanawasanifu.

Huyu juha mchuna mabuzi aliishiwa kujichuna na akaishia kujuta kwa kukumbuka blanketi asubuhi.

Ushauri wetu ni kwamba wote wenye tabia hizi waache. Waache uvivu na unyonyaji. Tafuteni kwa haki. Mtakula kwa furaha. Tamaa mbele mauti nyuma. Hivi ndivyo chunaji lilivyozidiwa akili na buzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *