Shinyanga. Watu 63 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma ya kujihusisha na matukio ya uhalifu ukiwemo wizi wa lita 295 za dizeli, mifuko 13 ya mawe yanayodhaniwa kuwa ya madini na noti za bandia zinazohesabika kama Sh81, 000.

Akitoa taarifa ya matukio hayo leo Aprili 28, 2026 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika matukio mbalimbali kwenye operesheni iliyofanyika Aprili ili kubaini na kuzuia uhalifu.

Magomi amesema vitu vingine vilivyokamatwa ni pamoja na pikipiki 14, simu 98 na betri za simu 86, bangi gramu 1,100 mirungi kilogramu 103, pombe ya moshi lita 55 na vipande 21 vya chuma.

“Operesheni hii imefanyika kwa mwezi mmoja katika Wilaya za Kahama na Ushetu na kukamata watuhumiwa 63 na vielelezo, lengo ni kuhakikisha tunabaini na kuzuia uhalifu,” amesema Magomi.

Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limefanikiwa kubaini makosa 4,260 kwa madereva wasiotii sheria za barabarani na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesema katika operesheni hiyo makosa ya magari ni 3,030 na makosa ya bajaji na pikipiki ni 1,230.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *