Paris, Ufaransa. Mabingwa watetezi wa Ulaya, Paris Saint-Germain, wanatarajiwa kuvaana na mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich, katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo usiku jijini Parishuko Ufaransa.
Bayern Munich inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa na rekodi nzuri baada ya kutwaa taji hili mara sita huku PSG ikilitwaa mara moja.
Timu hizi mbili zimezoeleka kuwa na mechi zenye ushindani mkali, baada ya zote kufuzu hatua hii kwa kuwaondoa vigogo wakubwa, PSG wakiitoa Liverpool huku Bayern wakiiondosha Real Madrid.
Kila timu imefunga mabao 38 katika mashindano ya msimu huu, idadi kubwa kuliko timu nyingine yoyote, hali inayoongeza hamasa kuelekea pambano hili.
Nyota wa PSG, Khvicha Kvaratskhelia wakati akipiga mpira katika moja ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
PSG wanahitaji ushindi ili kufika fainali kwa mara ya pili mfululizo, lakini watakutana na kigingi kigumu dhidi ya Bayern ambao wamekuwa mwiba kwao katika misimu ya hivi karibuni.
Ushindi wa mabao 2-1 wa Bayern katika hatua ya makundi msimu huu uliendeleza rekodi yao ya ushindi wa mechi tano mfululizo dhidi ya Mabingwa hao wa Ufaransa.
Hata hivyo, PSG wanaweza kujipa matumaini kutokana na uzoefu wa msimu uliopita ambapo walipoteza mapema dhidi ya Arsenal, lakini wakarejea kwa nguvu hatua za mtoano na hatimaye kuwatupa nje.
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane ambaye hadi sasa ameshapachika mabao 12 katika mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Picha na Mtandao
Vita ya nyota uwanjani
Macho yote yatakuwa kwa nahodha wa PSG, Marquinhos, ambaye anakaribia kufikisha mechi 120 katika Ligi ya Mabingwa, akilingana na rekodi ya Mbrazili mwenzake Roberto Carlos ambaye kwa sasa ameachana na soka. Atakutana na mshambuliaji hatari wa Bayern, Harry Kane, ambaye tayari amefunga mabao 12 msimu huu na kufunga katika mechi tano mfululizo za mashindano hayo.
Nahodha wa PSG, Marcos Aoás Corrêa ‘Marquinhos’ ambaye leo anakwenda kufikisha idadi ya mechi 120 za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Takwimu muhimu
Huu utakuwa mchezo wa 16 kati ya timu hizi kwenye Ligi ya Mabingwa, ambapo Bayern wanaongoza kwa ushindi mara tisa dhidi ya sita za PSG. Bayern pia wameshinda mechi tano zilizopita kati yao, ikiwemo ushindi wa 2-1 jijini Paris msimu huu.
PSG wamefanikiwa kufika nusu fainali kwa misimu mitatu mfululizo, rekodi ambayo haijawahi kufikiwa na klabu yoyote ya Ufaransa. Kwa upande mwingine, Bayern wanacheza nusu fainali kwa mara ya 22 katika historia yao, wakishinda 11 kati ya hizo.
Kocha wa PSG, Luis Enrique akizungumza kuelekea katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich. Picha na Mtandao
Makocha wanasemaje!
Kocha wa PSG, Luis Enrique, amesema timu yake bado inaendelea kukua licha ya kuwa mabingwa watetezi. Naye mshambuliaji Ousmane Dembélé amesisitiza kuwa wana njaa ya mataji zaidi.
Kwa upande wa Bayern, kocha Vincent Kompany amesema wanakabiliwa na changamoto kubwa lakini wana imani ya kufanya vizuri. Kiungo Joshua Kimmich ameongeza kuwa timu bora barani Ulaya sasa zinakutana katika hatua hii.
Baada ya mchezo huu, kesho kutakuwa na mechi nyingine kali ya hatua ya nusu fainali kati ya Atletico Madrid ambao watavaana na Arsenal kesho nchini Hispania.