Kila ifikapo Aprili 28, Tanzania na dunia huadhimisha Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani. Siku hii ni fursa ya kutafakari hali halisi ya usalama kazini na kupima mafanikio pamoja na changamoto zilizopo.

Pia, ni jukwaa la kuhimiza uwekezaji katika mifumo ya usalama, mafunzo, na teknolojia ili kupunguza vihatarishi mahali pa kazi.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Mazingira Bora ya Kazi Kisaikolojia ni Njia ya Kujenga Ustawi wa Wafanyakazi na Taasisi Imara,” inaakisi mabadiliko muhimu katika namna tunavyoelewa usalama na afya kazini.

Inaonesha wazi kuwa ustawi wa mfanyakazi hauishii kwenye kuepuka majeraha ya mwili pekee, bali unahusisha pia afya ya akili, hisia, na mahusiano kazini.

Jukwaa limehamia Njombe

Kitaifa, maadhimisho haya mwaka huu yanafanyika mkoani Njombe, yakiwa chini ya uratibu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), taasisi iliyokasimiwa dhamana hiyo kwa niaba ya Serikali. 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda akitoa tuzo ya usalama kazini kwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) baada ya kuibuka washindi kwenye tuzo hizo kwa upande wa taasisi za Serikali.

Katika maadhimisho haya, shughuli mbalimbali zinafanyika ikiwemo maonesho ya teknolojia na vifaa vya usalama na afya mahali pa kazi, mafunzo ya usalama na afya kwa wafanyakazi wa Taasisi za serikali na binafsi pamoja na makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo. Shughuli nyingine zinazofanyika kama sehemu ya maadhimisho haya ni bonanza la michezo na kuwatambua waajiri wanaotekeleza ipasavyo Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura Na. 297, Toleo la mwaka 2023.

Aidha, jukwaa la Njombe linatoa nafasi kwa Serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo kutathmini mafanikio yaliyofikiwa na kujadili changamoto zilizopo katika utekelezaji wa sera za usalama na afya mahali pa kazi. Kupitia shughuli hizi, mikakati mipya huibuliwa ili kuimarisha zaidi ulinzi wa afya na usalama wa wafanyakazi nchini.

Maonyesho hayo yananogeshwa na zoezi la ugawaji Tuzo za Usalama na Afya zinazoandaliwa na OSHA. Tuzo hizo hutolewa kutambua mchango wa taasisi na watu binafsi waliofanikiwa kusimamia usalama mahala pa kazi. Utambuzi huu hutoa motisha kwa taasisi nyingine kuiga mfano wa wale wanaoibuka washindi.

Uboreshaji afya ya akili kwa wafanyakazi

Kama ambavyo kauli mbiu inavyosema, OSHA imewekeza nguvu katika kuboresha afya ya kisaikolojia kwa wafanyakazi wengi ili waweze kustawi.

Katika ulimwengu wa kazi wenye kasi na ushindani mkubwa, changamoto kama msongo wa mawazo, uchovu uliopitiliza na unyanyasaji kazini, imekuwa jambo la kawaida.

Hivyo, OSHA imeendelea kuweka msisitizo kwa waajiri kuboresha mazingira ya kazi ili yawape faraja na ari badala ya kuwaletea uchovu na msongo wa mawazo.

Hatua hii inakwenda kubadili mtazamo wa waajiri wengi juu ya dhana ya usalama na afya, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitazamwa tu pale mfanyakazi anapoathirika kimwili na si kihisia au kiakili.

Mfanyakazi anayejisikia kuthaminiwa na kulindwa kisaikolojia huwa mbunifu zaidi, mzalishaji zaidi, mwenye ari na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto. Hapa ndipo daraja kati ya ustawi wa mfanyakazi na mafanikio ya taasisi linapojengwa.

Usalama na sekta nyingine za kiuchumi

Nchini Tanzania, sekta ndogo za uchumi maarufu kama sekta isiyo rasmi, ndizo zinazobeba sehemu kubwa ya ajira na kipato kwa wananchi wengi. Kuanzia mafundi seremala, mama lishe, wachomeleaji, hadi wachimbaji wadogo, sekta hii ni injini ya maisha ya kila siku.

Baadhi ya wafanyakazi wakiandamana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Aprili 28.

Hata hivyo, pamoja na mchango wake mkubwa, masuala ya usalama na afya mahali pa kazi bado hayajapewa kipaumbele kinachostahili.

Changamoto kubwa katika sekta hizi ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu vihatarishi vya kazi na namna ya kujilinda. Wafanyakazi wengi hufanya kazi bila vifaa kinga, katika mazingira yasiyo salama, na bila mwongozo rasmi wa usalama.

Katika kukabiliana na hali hii, OSHA imekuwa ikipanua wigo wa uelimishaji kwa kulenga makundi haya. Kupitia mafunzo ya vitendo, kampeni za uhamasishaji, na ushirikiano na serikali za mitaa, OSHA inawafikia wajasiriamali wadogo na kuwapa mbinu rahisi na nafuu za kuboresha usalama wao kazini.

Usalama ni jukumu la kila mmoja

Usalama ni jukumu la kila mmoja, lakini hilo haliwezi kutokea bila mfumo imara wa sera na usimamizi. Ndiyo maana nafasi ya Serikali ni ya msingi katika kuweka mwelekeo, viwango, na uwajibikaji.

Hata hivyo, sera pekee hazitoshi bila utekelezaji madhubuti. Ni muhimu kuwe na ukaguzi wa mara kwa mara, utoaji wa adhabu kwa wanaokiuka sheria, na motisha kwa wanaozingatia viwango vya usalama. Hii inasaidia kujenga uwajibikaji na kuhakikisha kuwa usalama hauchukuliwi kama chaguo bali kama lazima.

Kwa upande mwingine, waajiri wanapaswa kuwajibika moja kwa moja kwa kuweka mazingira salama ya kazi, kutoa mafunzo, na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa kinga. Wafanyakazi nao wanapaswa kufuata taratibu za usalama na afya na kutoa taarifa za vihatarishi bila kusita.

Kwa ujumla, usalama bora kazini unatokana na muunganiko wa mambo mawili: sera thabiti kutoka serikalini na uwajibikaji wa kila mmoja mahali pa kazi. Bila ushirikiano huu, juhudi za kulinda maisha na afya ya wafanyakazi haziwezi kufikia matokeo yanayotarajiwa.

Usalama ni chachu ya maendeleo ya Taifa

Hakuna maendeleo endelevu yanayoweza kupatikana bila kuwepo kwa mazingira salama yanayolinda maisha, afya, na utu wa watu.

Hapa nchini, nguvu kazi ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi. Wafanyakazi wanapokuwa salama na wenye afya njema, uzalishaji huongezeka, ubora wa kazi huimarika, na gharama zinazotokana na ajali au magonjwa hupungua. Hii ina maana kuwa usalama si tu suala la kibinadamu, bali pia ni mkakati wa kiuchumi unaochochea maendeleo ya Taifa.

Kupitia OSHA, mazingira ya kazi yanapoboreshwa, yanaweka msingi wa uwekezaji na ukuaji wa sekta mbalimbali. Wawekezaji huvutiwa zaidi na nchi zenye mifumo imara ya kulinda afya na usalama wa wafanyakazi, kwani hupunguza hatari za uzalishaji na kuongeza ufanisi.

Mwisho wa yote, ni vyema kujiuliza: maendeleo tunayoyatafuta yana maana gani kama hayalindi maisha ya anayeyachochea? Kila kiwanda kinapozalisha, kila shamba linapovunwa, na kila huduma inapotekelezwa, kuna mkono wa mfanyakazi nyuma yake na mkono huo unastahili ulinzi, heshima, na uthamini.

Kuelekea uchumi imara na wa kisasa hususan katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inatekeleza Dira ya Taifa ya 2050, lazima jitihida hizi ziendane na dhamira ya dhati ya kuweka usalama mbele. Kupitia juhudi za taasisi kama OSHA, msingi umewekwa lakini mafanikio ya kweli yatatokana na hatua za kila mmoja wetu.

Usalama usibaki kuwa sera kwenye karatasi au kauli mbiu kwenye maadhimisho. Uwe utamaduni, unaotafsiriwa kwa vitendo kila siku, katika kila eneo la kazi. Kwa sababu mwisho wa siku, mafanikio ya Taifa hayapimwi tu kwa ukuaji wa uchumi, bali kwa namna yanavyolinda uhai, utu, na ndoto za watu wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *