Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepoteza mkongwe wake mwingine, Maulida Anna Komu, huku baadhi ya waliowahi kufanya naye kazi wakimkumbuka kwa kupigania haki na umakini katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa mujibu wa ndugu wa Anna Komu, Salum Mwalimu, ameliambia Mwananchi leo Jumanne, Aprili 29, 2026, kuwa mama yake mkubwa huyo amefariki dunia jana kati ya saa nne na tano usiku, wakati akipatiwa matibabu Mjini Unguja.

“Atazikwa leo alasiri, na maziko yatakuwa Kisiwandui, Msikiti Mabati. Alikuwa akiugua kwa muda kidogo, ‘of course’ amekuwa akiumwaumwa kwa muda sasa, ile kuumwa na kulazwa hospitali ni karibu wiki tatu sasa,” amesema Mwalimu ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Kifo cha Komu, aliyekuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Chadema, kimetokea siku mbili baada ya chama hicho kumpoteza aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Dk Medard Mutungi, aliyefariki dunia Aprili 26, 2026.

Wanavyomzungumzia

Waliowahi kufanya kazi na Komu wanamtaja kuwa ni mwanamke jasiri, mwenye msimamo na aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za siasa za mageuzi tangu mwishoni mwa miaka ya 1980.

Wanasema Anna Komu atakumbukwa kwa ujasiri, uthubutu na kujitoa kwake katika kuijenga Chadema hadi kuwa chama chenye ushawishi mkubwa nchini, sambamba na kupigania Watanzania.

Kada wa zamani wa Chadema, Basil Lema, ameliambia Mwananchi kuwa alipata kigugumizi baada ya kusikia taarifa za kifo cha Maulida kwa kuwa kwake alikuwa kama mama yake.

“Tumekaa nyumba moja kwa baba yangu huku Kilimanjaro, pamoja na mengine yote nilimchukulia kama mama. Namfahamu Maulida kama mtu makini, akiamua jambo atalifanya kwa weledi na hakuna wa kumzuia,” anasema Lema.

Mbali na hilo, Lema anaeleza kuwa Maulida alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza walioshiriki harakati za siasa za mageuzi kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1980 na kuendelea.

Lema anasema Maulida, akiwa ameweka kambi Moshi, alishika wadhifa wa ukatibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro (wa kwanza) katika miaka ya 1990 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.

“Zile enzi za kuhutubia miti (bila watu), watu walikuwa wakikataa Chadema. Mnafanya mkutano ulioandaliwa kwa gharama kubwa, lakini hakuna watu au mnapata wahudhuriaji saba.

“Ilikuwa shughuli kwa kweli, lakini Maulida akiwa na Ndesamburo (Philemon) walipambana na kwa mara ya kwanza mwaka 1995 Chadema kilipata mbunge mmoja (Rombo) katika Mkoa wa Kilimanjaro. Wakati huo NCCR-Mageuzi ndicho chama kilichokuwa na nguvu zaidi,” anasema.

Akiwa na wadhifa huo, mwaka 2000 Mkoa wa Kilimanjaro ulipata wabunge kama kina Ndesamburo (Moshi Mjini) na Freeman Mbowe (Hai), ingawa majimbo mengine yalikwenda CCM na NCCR-Mageuzi.

Lema anaeleza kuwa baada ya kutoka Kilimanjaro, Maulida alihamia Dar es Salaam na alifanikiwa kujenga chama hasa Kinondoni, ambako Chadema haikupendwa, na maeneo yenye upinzani CUF ndiyo ilikuwa ikipendwa.

Kwa mujibu wa Lema, mwaka 2005, baada ya mgombea mwenza wa urais wa Chadema, Jumbe Rajab Jumbe, kufariki dunia zikiwa zimesalia siku nne kabla ya Uchaguzi Mkuu uliomweka madarakani mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, kifo hicho kilisababisha uchaguzi huo kusimamishwa kwa muda, na Rais Benjamin Mkapa (hayati), aliyekuwa amalize muda wake Novemba, kulazimika kuendelea na wadhifa huo hadi Desemba.

Lema anasema baada ya kifo hicho, Kamati Kuu ilimteua Maulida kuwa mgombea mwenza, na walifanya kazi kubwa na Mbowe akienda Magharibi, naye akienda Mashariki.

“Lengo halikuwa kuchukua urais, bali kusimika na kuimarisha chama, na kazi hiyo ilifanikiwa. Ndiyo maana leo Chadema kipo kila sehemu,” anasema Lema.

Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, anasema kipindi chote cha uhai wake Anna Komu alikuwa mpambanaji katika kuhakikisha haki na demokrasia inapatikana nchini.

“Ni mtu aliyeshiriki misheni mbalimbali za kuhakikisha haki inapatikana. Ameutumia umri wake wote kupigania haki. Hata leo kifo kimemfikia akiwa katika mapambano ya kutafuta haki, hasa upande wa Zanzibar,” anasema.

Said anasema Maulida alikuwa akishirikiana na makundi yote na mara ya mwisho kuzungumza naye ilikuwa kwenye kesi ya mgawanyo wa mali walioifungua mapema mwaka huu.

“Ni mama wa mfano, alikuwa kwenye harakati tangu Chadema inaasisiwa na popote watu waliposhindwa kuthubutu, Maulida alithubutu. Nakumbuka mwaka 2005 alivyowania ugombea mwenza wa urais,” anasema.

Anasema atamkumbuka kwa namna alivyokuwa akieleza kuhusu kesi ya madai ya mgawanyo wa mali kuwa yeye na wenzake hawana ugomvi na Chadema, bali wanataka haki sawa kila upande.

“Alikuwa akisema kinachotakiwa Chadema wakubali tatizo lililopo ili tupate ufumbuzi na kesi iondoke. Alisisitiza uwiano uwepo baina ya Tanzania bara na Zanzibar kuhusu mgawanyo wa mali.

“Alituambia ukizungumza uwiano, maana si sawa kwa sawa, angalau kwenye magari 40 basi Zanzibar ipate hata mawili tu. Huu ndio ulikuwa msimamo wake Anna Komu,” anasema Said.

Usioyajua kuhusu Maulida Komu

Maulida Komu alijiunga Chadema mwaka 1993 akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu wakati huo alipata nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Miongoni mwa nafasi alizowahi kushika ni ubunge wa viti maalumu, Waziri Kivuli wa Maendeleo ya Jamii, makamu mwenyekiti wa bodi ya wadhamini na baadaye alikaimu nafasi ya mwenyekiti wa bodi hiyo baada ya kifo cha aliyekuwa mwenyekiti, Sylvester Masinde.

Hata hivyo, mwaka 2026 Maulida na wajumbe wengine wa bodi ya wadhamini, Ahmed Rashid Khamis na Said Issa Mohamed, walifungua kesi ya mgawanyo wa mali za Chadema, shauri la mwaka 2025.

Katika kesi hiyo, waliomba mahakama izuie chama kufanya shughuli za kisiasa na viongozi wake kuzuiwa kutumia mali za chama.

Mahakama Kuu iliweka zuio kwa viongozi wa Chadema kufanya shughuli zozote za kisiasa na waliokuwa wakijaribu kufanya hata vikao vya ndani.

Pia, mahakama hiyo ilizuia mali za Chadema zisiguswe, hatua iliyosababisha ofisi na magari ya chama hicho kukaa muda mrefu bila kutumika.

Amri hiyo ilidumu takribani mwaka mmoja kabla ya kufutwa na Mahakama ya Rufani Aprili 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *