Kibiti. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa ametangaza hatua kali dhidi ya watumishi wa afya watakaoshindwa kutoa huduma kwa wajawazito kwa kisingizio cha kukosa fedha za matibabu, akisisitiza kuwa uzembe huo hautavumiliwa na unaweza kusababisha kupoteza ajira pamoja na leseni za taaluma.
Amesema licha ya Tanzania kupiga hatua katika kupunguza vifo vya wajawazito kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2022, bado changamoto ya uzembe na vitendo vya rushwa miongoni mwa baadhi ya watoa huduma inaendelea kuchangia vifo hivyo.
Akizungumza leo Jumatano, Aprili 29, 2026, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yaliyofanyika wilayani Kibiti, mkoani Pwani, Mchengerwa amesema serikali haitakubali kuona mjamzito akipoteza maisha au kupata madhara kutokana na kucheleweshwa au kunyimwa huduma muhimu hospitalini.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, akimpatia mtoto mchanga matone ya vitamini (chanjo) wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
“Sitakubali kusikia mama mjamzito analazwa sakafuni au anazuiwa kupata huduma kwa sababu hana fedha, au anapoteza maisha kwa kukosa huduma kwa wakati. Huu si uzembe tu, bali ni ukiukwaji wa haki ya msingi ya Mtanzania kupata huduma bora za afya,” amesema kwa msisitizo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema waganga wakuu wa mikoa na halmashauri watakaoshindwa kusimamia upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya watachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nafasi zao.
Amesema serikali kwa kushirikiana na Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, imekubaliana kuwa hakuna sababu ya wananchi kukosa dawa wakati takwimu zinaonyesha upatikanaji wake umefikia asilimia 90.
“Upatikanaji wa dawa haupaswi kubaki kwenye takwimu za makaratasi, bali uonekane kwa mgonjwa anayefika kituoni. Mgonjwa anayekosa dawa anakosa si tiba tu, bali pia haki yake ya msingi,” amesema.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, akizungumza kuhusu huduma za chanjo nchini. Kulia ni Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Profesa Mary Nagu.
Katika jitihada za kuboresha huduma za afya, Mchengerwa amesema serikali imejikita katika kusogeza huduma karibu na wananchi ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.
Ametolea mfano ujenzi wa hospitali ya mkoa itakayohudumia wananchi wa Rufiji, Kibiti na Mkuranga, hatua itakayopunguza utegemezi wa hospitali za Temeke mkoani Dar es Salaam na Kibaha Mkoa wa Pwani.
“Wananchi hawapaswi kusafiri kilomita 300 au 400 kupata huduma za msingi. Tunajenga miundombinu hii ili huduma zipatikane karibu, isipokuwa kwa matibabu ya kibingwa,” amesema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, serikali imejenga vituo vya afya zaidi ya 3,500 na kuimarisha miundombinu ya sekta hiyo kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wakati.
Mbali na hilo, Mchengerwa amesema mpango wa serikali kuanza kuzalisha chanjo ndani ya nchi katika eneo la Mloganzila, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi wa nje na kuimarisha sekta ya afya.
“Tunatoka katika uzalishaji wa dawa kwa asilimia 16 na tunaelekea kufikia asilimia 80. Zaidi ya kampuni 60 kubwa duniani zimeonyesha nia ya kuwekeza nchini katika uzalishaji wa dawa,” amesema.
Hata hivyo, ameonya kuwa mafanikio hayo hayatakuwa na tija iwapo vitendo vya rushwa, uzembe na unyanyasaji wa wagonjwa vitaendelea kuwepo miongoni mwa watumishi wa afya.
“Yapo mambo ya kufanyia mzaha, lakini afya ya Mtanzania siyo mojawapo. Tutachukua hatua kali, ikiwemo kufuta leseni za wahusika,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe amesema magonjwa mengi yanayolikumba taifa yanatokana na ukosefu wa elimu ya afya, hususan katika masuala ya lishe na usafi wa mazingira.
Amesema serikali inaendelea kutoa huduma kupitia kampeni za Mkoba katika vituo zaidi ya 8,600, zikijumuisha chanjo, uchunguzi wa magonjwa na utoaji wa elimu ya afya kwa jamii.
“Afua nyingi za afya zinaanzia kwenye kinga. Tunapaswa kuwekeza zaidi katika elimu ya lishe bora na usafi wa mazingira ili kupunguza mzigo wa magonjwa yanayozuilika,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia afya katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Mary Nagu amesema serikali imewekeza zaidi ya Sh1.34 trilioni katika kuboresha miundombinu ya afya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa hospitali 127 na vituo vya afya zaidi ya 360.
Amesema uwekezaji huo umeongeza upatikanaji wa huduma za upasuaji, ikiwemo upasuaji wa dharura wa kumtoa mtoto tumboni, na kuchangia ongezeko la wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 61 mwaka 2020 hadi asilimia 81 kwa sasa.
Kwa upande wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya amesema serikali imewekeza Sh1.06 trilioni katika kuimarisha sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali za mikoa na upanuzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja pamoja na hospitali ya kufundishia Zanzibar.
Kwa ujumla, viongozi hao wamesisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya afya hayatategemea uwekezaji wa miundombinu pekee, bali pia nidhamu, uwajibikaji na maadili ya watumishi wa afya katika kuwahudumia wananchi.
Mchengerwa amehitimisha kwa kusisitiza kuwa serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utoaji wa huduma za afya ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayenyimwa haki yake ya kupata matibabu bora.