
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran amesema kuwa Marekani haina tena uwezo wa kulazimisha sera zake kwa mataifa huru, akiongeza kuwa hali hiyo sasa imejidhihirisha wazi duniani kupitia ustahimilivu wa wananchi wa Iran pamoja na vikosi vyake vya ulinzi.
Brigedia Jenerali Reza Talaei-Nik, akizungumza alipowasili Bishkek, Kyrgyzstan, kushiriki mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO), alisisitiza umuhimu wa kuendeleza msimamo thabiti wa jeshi la Iran pamoja na mfano wa ustahimilivu wa wananchi wake katika jukwaa la kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, alisema: “Marekani si tena katika nafasi ya kulazimisha sera zake kwa mataifa huru.”
Aliongeza kuwa hali hiyo “imebainika kwa ulimwengu mzima kupitia uvumilivu na uthabiti wa watu wa Iran pamoja na vikosi vyao vya ulinzi. Hatimaye Marekani italazimika kukubali kuachana na madai yake yasiyo halali na yasiyo na mantiki.”
Talaei-Nik aliendelea kusema kuwa sasa dunia nzima inazitambua Marekani pamoja na utawala wa Israel kama “alama za ugaidi wa kiserikali.”
Alisema kuwa “uhalifu wao wa wazi katika kuwaua wasio na hatia, hususan watoto na wanafunzi wa shule ya Minab, umeharibu kabisa uaminifu wa dunia ya Magharibi kuhusu maadili wanayodai kuyasimamia.”
Msemaji huyo pia alithibitisha utayari kamili wa vikosi vya ulinzi vya Iran kukabiliana na hatua yoyote ya makosa ya kimkakati kutoka kwa maadui wake.
Amesisitiza: “Leo hii, huku tukiwa na utayari kamili wa kujihami kwa nguvu na kukidhi mahitaji ya vikosi vyetu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kushirikiana uwezo wake wa ulinzi na kijeshi na mataifa huru, hasa yale wanachama wa SCO.”
Aidha, aliielezea SCO kama ishara ya dhamira ya mataifa na serikali kujinasua kutoka mfumo usio wa haki wa dunia unaotawaliwa na upande mmoja, kuelekea mfumo wa nguvu nyingi zaidi duniani.
Mara tu baada ya kuwasili Bishkek, Talaei-Nik alifanya mikutano ya kando na mawaziri wa ulinzi wa Kyrgyzstan, Russia, Pakistan na Belarus, mataifa yenye ushawishi mkubwa ndani ya SCO.