Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa onyo kali kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara wilayani humo, akiwataka kuzingatia mikataba na kukamilisha kazi kwa wakati ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.
Mpogolo ametoa onyo hilo leo Alhamis Aprilu 30, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya barabara aliyoifanya kwa kushirikiana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, ambapo ametembelea miradi inayotekelezwa na wakandarasi mbalimbali, wengi wao wakiwa wazawa.
Akizungumza katika ziara hiyo, amewakosoa baadhi ya wakandarasi kwa kuchelewesha miradi kwa visingizio visivyo na msingi, akisema hali hiyo inawaumiza wananchi huku Serikali ikiwa tayari imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo.
“Serikali imetoa fedha, hakuna sababu ya kuchelewesha miradi. Wananchi wanahitaji huduma bora na kwa wakati,” amesema Mpogolo.
Aidha, ameonya tabia ya baadhi ya wakandarasi kukaidi maelekezo ya wasimamizi wa miradi kutoka TARURA na TANROADS, wakitumia mwanya wa kufahamiana na baadhi ya viongozi wa juu.
Amesisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa, hasa vinapoambatana na ujenzi wa barabara chini ya viwango vilivyokubaliwa kwenye mikataba.
Mbali na hilo, Mpogolo ameeleza wasiwasi wake juu ya wakandarasi wanaochukua miradi mingi kwa wakati mmoja bila kuwa na rasilimali na vifaa vya kutosha, jambo linalochangia baadhi yao kutelekeza miradi au kuchelewesha utekelezaji wake.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uchunguzi wa miradi kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi wanaokiuka taratibu na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Katika ziara hiyo, ametaja baadhi ya barabara zilizokaguliwa kuwa ni Halisi na Kimanga, zilizogharimu Sh1.7 bilioni zilizotolewa mwaka 2024.
Barabara nyingine ni Mafia, Masasi, Magila, Bondi na Muhonda zilizogharimu Sh1.8 bilioni mwaka 2025, pamoja na Mwanza, Livingstone, Nyamwezi, Kipati, Msikitini, Sharifushamba, Kigoma na Tunduru zilizogharimu Sh1.9 bilioni.
Mpogolo amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaoathiri ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa lengo kuu ni kuboresha miundombinu na kuinua maisha ya wananchi.