Dar es Salaam. Mara nyingine Diamond Platnumz amekubali kuimba Singeli baada ya hilo kusubiriwa kwa muda mrefu na mashabiki wake baadhi waliotamani kumsikia tena katika aina hiyo ya muziki unaovuma zaidi uswahilini.
D Voice, mwanamuziki wa mwisho kutambulishwa WCB Wasafi, ndiye amemshirikisha Diamond katika wimbo wake mpya wa Singeli, Iyo (2026) uliotayarishwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic.
Hii inakuwa mara ya pili kwa wawili hao kushirikiana, tena katika ngoma ya Singeli baada ya hapo awali Diamond kusikika katika wimbo wa D Voice ‘Kama Wengine’ unaopatikana katika albamu yake, Swahili Kid (2023).
Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2010, muziki wa Singeli ulianza kujizoelea umaarufu na hatimaye kutengeneza mastaa wake kama Msaga Sumu, MC Sudi, Dulla Makabila, Man Fongo, Meja Kunta, Sholo Mwamba n.k.
Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) zilizoanzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa Taifa (Basata), ziliijumuisha Singeli kuanzia msimu wa 2021 na hii ni kwa sababu ya ushawishi wake.
Umaarufu wa Singeli uliwavutia mastaa wengi wa Bongo Fleva kama Professor Jay, Harmonize, Rayvanny, Alikiba, Jux na Zuchu, ambao nao kwa nyakati tofauti waliamua kutoa nyimbo za mahadhi yao na nyingi zilipokelewa vizuri.
Mathalan Harmonize aliachia wimbo wake wa Singeli, Hajanikomoa (2020) na video yake kuwa ya kwanza katika aina hiyo ya muziki kutazamwa (views) mara milioni 1 YouTube ndani ya wiki moja.
Rayvanny, muda mfupi baadaye akaachia video yake ya Singeli, Miss Buza (2020) akiwa na Dulla Makabila, ambayo ilitazamwa YouTube mara milioni 1 ndani ya siku moja na hadi sasa imefikia milioni 14.
Staa huyo wa Next Level Music (NLM) hakuishia hapo, akatoa wimbo mwingine wa Singeli akiwa na DJ Misso Misondo, Kitu Kizito (2023) ambao ulikuja kushinda tuzo ya TMA kama Wimbo Bora wa Singeli 2023.
Hata hivyo, kwa Diamond mambo ni tofauti kidogo linapokuja suala la miondoko ya Singeli. Nyimbo zake zote alizoimba ameshirikishwa tena na msanii wake wa WCB Wasafi, D Voice. Hivyo Diamond hajatoa wimbo wake binafsi wa Singeli.
Pengine Diamond hajapenda kujitoa moja kwa moja katika Singeli au anaona akifanya kazi na D Voice kwa upande wake inatosha kwa sababu msanii huyo tayari ana ushawishi upande huo kwa miaka mingi.
Utakumbuka kabla ya D Voice kusainiwa WCB Wasafi, tayari alikuwa ameshavuma katika Singeli kupitia wimbo wake maarufu, Kuachana Shingapi (2021), ambao alitoa hadi remix yake akiwa na Platform, Lody Music na Barnaba.
Huyu ni msanii wa kwanza anayeimba Singeli kusainiwa na WCB Wasafi, rekodi lebo yake Diamond ambayo ndani ya miaka 10 tayari imewasimamia wasanii wanane tena kwa mafanikio.
Mbali na D Voice, msanii mwingine wa WCB Wasafi anayefanya vizuri Singeli ni Zuchu ambaye wimbo wake wa kwanza ni Nyumba Ndogo (2021) ambao unashikilia rekodi kama wimbo wa Singeli Bongo ambao video yake imefanya vizuri YouTube ikitazamwa mara milioni 46.
Baada ya hapo Zuchu alikuja na wimbo mwingine wa Singeli akiwa na D Voice ‘Hujanizidi’ ambao ulijumuishwa katika albamu yake ya kwanza, Peace and Money (2023).
Wakati D Voice, Zuchu na mastaa wengine wa Bongo Fleva wakipiga ngoma za Singeli, Diamond aliweka nguvu kubwa katika muziki wa Amapiano ambao asilimia yake ni Afrika Kusini.
Tayari Diamond amevuma na nyimbo zake za Amapiano kama Iyo (2021), Shu! (2023), Komasava (2024) na Sasampa (2025) na zote zimeshirikisha wasanii kutoka Afrika Kusini.
Kati ya yote hizo, Komasava ndiyo ulifanya vizuri zaidi hadi kuingia chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs, ukiwa ni wimbo wa kwanza kutoka Tanzania kufanya hivyo, hadi sasa hakuna wimbo mwingine ulioweza kufikia rekodi hiyo.
Ikumbukwe wimbo huo uliingia moja kwa moja hadi nafasi ya 39 kati ya nyimbo 50, huku wimbo wa mshindi wa Grammy 2024 kutoka Afrika Kusini, Tyla, Water (2023) ukishika nafasi ya kwanza.
Chati ya Billboard U.S Afrobeats Songs inatoa orodha ya nyimbo 50 za kutoka Afrika hasa zenye mahadhi ya Afrobeats ambazo ni maarufu Marekani katika majukwaa ya kidijitali ya kusikiliza muziki.