
Dar es Salaam. Serikali imepanga kutumia Sh103.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao unatajwa kuwa uti wa mgongo wa huduma za kidijitali nchini.
Akiwasilisha mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Alhamisi, Aprili 30, 2026, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema miongoni mwa kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuunganisha Mkongo wa Taifa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hatua itakayoongeza wigo wa mawasiliano ya kikanda na kurahisisha biashara na uwekezaji.
Aidha, vituo 20 vitaunganishwa kwenye mkongo huo huku Serikali ikipanga kujenga vituo viwili vya kisasa vya kuhifadhi data (Data Centres) katika mikoa ya Dodoma na Zanzibar ili kuongeza usalama na uhifadhi wa taarifa za kidijitali.
Katika kuimarisha huduma za intaneti, amesema wizara itasimamia vituo saba vya mabadilishano ya intaneti (Internet Exchange Points) pamoja na kuwezesha huduma za Wi-Fi katika maeneo 100 ya umma nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mtandao kwa wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wa sekta ya elimu amesema shule 100 zitaunganishwa na huduma ya mkongo kupitia maunganisho ya mwisho, jambo litakalosaidia wanafunzi na walimu kupata rasilimali za kujifunzia kwa njia ya mtandao.
Serikali pia imepanga kuimarisha miundombinu ya taarifa muhimu za kitaifa katika maeneo 100 ya umma pamoja na kuboresha Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam.
Hatua nyingine ni kuunganisha taasisi 100 za haki jinai na ulinzi na usalama, zikiwemo mahakama, polisi, magereza na taasisi za kupambana na rushwa, ili kuboresha utendaji kazi kwa kutumia mifumo ya kidijitali.
Pia, vifaa vya mikutano ya video vitasakinishwa na kuboreshwa katika wilaya 100 ili kurahisisha mawasiliano na uratibu wa shughuli za Serikali.
Waziri amesema utekelezaji wa miradi hiyo utakwenda sambamba na Mkakati wa Kitaifa wa Brodibendi na Mpango Kabambe wa Miundombinu, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kisasa unaotegemea Tehama.