KMC inapigania uhai wake wa kusalia Ligi Kuu Bara msimu ujao ikiwa pia bila kocha mkuu, huku uongozi wa klabu hiyo ukiweka wazi kuwa bado kuna hesabu zinaendelea kupigwa taratibu juu ya mchakato wa kupata kocha mpya.

Timu hiyo msimu huu imeshaachana na makocha wawili, akitangulia Marcio Maximo aliyeanza msimu na kikosi hicho, kisha akafuata Abdallah Mohamed ‘Baresi’. Kuondoka kwa makocha hao ni kutokana na timu hiyo kukosa matokeo mazuri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka, amesema hatma ya klabu hiyo kupata kocha mpya bado inahitaji subira kutokana na uongozi kupiga hesabu za ni kocha gani atawafaa kwa sasa.

Madenyeka amesema klabu hiyo inataka kufanya uamuzi sahihi katika kutafuta kocha huyo mpya ambapo vikao hivyo vitaendelea baada ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu Bara.

“Mchakato wa kocha mpya bado kidogo, tunaendelea kwanza kufanya tathmini ya tunaingiaje kwenye mchakato huo na kocha gani anatufaa kwa sasa kulingana na changamoto za timu yetu,” amesema Madenyeka.

“Tunataka kwanza kucheza mchezo wetu dhidi ya JKT, baada ya hapo tutarudi mezani tena kuangalia ni hatua gani tunatakiwa kuzichukua, kitu muhimu hapa ni kupata matokeo.”

KMC inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi tisa, huku ikiwa pia ndiyo timu iliyoshinda mechi chache zaidi, michezo miwili pekee, ikitoa sare tatu na kupoteza 14.

Timu hiyo kwa sasa inayonolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Imani Mwalupetelo ambapo jana ilikuwa uwanjani kucheza mchezo wake wa 20 msimu huu ndani ya Ligi Kuu Bara ikiwa ugenini dhidi ya JKT Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *