
Dar es Salaam. Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania imeendelea kuonesha kasi ya ukuaji huku takwimu mpya zikibainisha ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano ndani ya mwaka mmoja.
Akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya mawasiliano na teknoloaji ya habari, bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Aprili 30, 2026 Waziri Angellah Kairuki amesema idadi ya laini za simu zilizosajiliwa imeongezeka kutoka milioni 90.4 Machi 2025 hadi kufikia milioni 111.9 Machi 2026, sawa na ongezeko la asilimia 23.8.
Ongezeko hilo linakwenda sambamba na kuimarika kwa matumizi ya intaneti, ambapo watumiaji wameongezeka kutoka milioni 49.3 hadi milioni 58.9 katika kipindi hicho, sawa na ukuaji wa asilimia 19.5.
Katika huduma za fedha kwa njia ya simu, maarufu kama ‘mobile money’, amesema watumiaji wameongezeka kutoka milioni 66.5 hadi milioni 81.0, hatua inayotafsiriwa kuwa ongezeko la asilimia 21.8 na kuonesha namna huduma hizo zinavyoendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa kidijitali.
Mbali na ongezeko la watumiaji, pia kumeshuhudiwa ukuaji wa watoa huduma katika sekta hiyo. Waziri huyo amesema idadi ya watoa huduma wa miundombinu ya mawasiliano imefikia 52 Machi 2026 ikilinganishwa na 38 waliokuwepo Machi 2025, sawa na ongezeko la asilimia 36.8.
Aidha, watoa huduma za ziada (Application Services and Value-Added Services) wameongezeka kutoka 136 hadi 173 katika kipindi hicho, sawa na ongezeko la asilimia 27.2.
Akifafanua, Waziri amesema mafanikio hayo yanatokana na uwepo wa mifumo imara na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali, yanayolenga kukuza sekta ya Tehama na kuvutia uwekezaji zaidi.
“Takwimu hizi zinaonesha wazi kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano na teknolojia ya habari nchini,” amesema Kairuki.