
Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imetumia takribani dola za Marekani 25 bilioni (sawa na Sh62.5 trilioni) katika vita vinavyoendelea dhidi ya Iran, kwa mujibu wa ofisa mwandamizi wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon).
Hii ni mara ya kwanza kwa mamlaka za kijeshi za Marekani kutoa makadirio rasmi ya gharama za operesheni hiyo iliyoanza Februari 28, 2026, kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na Reuters na DW.
Vita kati ya Marekani, kwa kushirikiana na Israel, dhidi ya Iran vilianza Februari 28, 2026, ambapo mashambulizi ya kwanza yalikuwa ya anga, huku Marekani na Israel zikilenga kushambulia maeneo mbalimbali ndani ya Iran.
Operesheni hiyo iliyopewa jina la kijeshi ‘Epic Fury’, ilifuatiwa na hatua ya Iran kujibu mashambulizi kwa kurusha makombora na droni, ikilenga vituo vya kijeshi pamoja na maeneo ya washirika wa Marekani katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Ofisa huyo, Jules Hurst ameliambia Bunge la Marekani Jumatano Aprili 29, 2026, kupitia Kamati ya Huduma za Kijeshi, kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo zimetumika katika ununuzi wa silaha na risasi za kivita. Hata hivyo, hakutoa ufafanuzi wa kina kuhusu vipengele vyote vilivyojumuishwa katika hesabu hiyo, ikiwamo gharama za ujenzi upya wa miundombinu ya kijeshi iliyoharibiwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kauli hiyo ilipokewa kwa tahadhari na baadhi ya wabunge, akiwamo Adam Smith, kiongozi wa juu wa Chama cha Democratic katika kamati hiyo, ambaye amesema wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata takwimu rasmi za gharama za vita hivyo.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth ametetea matumizi hayo, akisisitiza kuwa ni muhimu katika kuhakikisha Iran haimiliki silaha za nyuklia.
“Utalipa kiasi gani kuhakikisha Iran haipati bomu la nyuklia?” amehoji Hegseth mbele ya wabunge.
Wakati huohuo, vita hivyo imeendelea kuwa na athari za kiuchumi duniani, hasa katika sekta ya nishati. Usafirishaji wa mafuta na gesi asilia umeathirika, hali iliyosababisha kupanda kwa bei za nishati katika maeneo mbalimbali, ikiwamo Tanzania.
Ndani ya Tanzania, kumeshuhudiwa ongezeko la Zaidi ya Sh900 kwa lita ya mafuta, ongezeko ambalo halijawahi kutokea kwa zaidi ya miaka 20. Hali hiyo imeongeza gharama za maisha, ikiwamo kupanda kwa nauli za usafiri wa mabasi na daladala, pamoja na gharama za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa na huduma.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, wanajeshi 13 wa Marekani wameripotiwa kupoteza maisha, huku mamia wakijeruhiwa katika mapigano hayo.
Licha ya kuwepo kwa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano, Marekani imeendelea kuimarisha uwepo wake wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, ikiwamo kupeleka maelfu ya wanajeshi pamoja na meli tatu za kubeba ndege za kivita.