Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema jumla ya hospitali 11 za rufaa za mikoa nchini, zinatarajia kuanza kutoa huduma za uchujaji wa damu (dialysis) kwa wenye magonjwa sugu ya figo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Dialysis ni matibabu ambayo kawaida hujumuisha kutumia mashine kuchukua kazi ya figo kuchuja sumu, taka na maji kupita kiasi kutoka mwilini. Tiba hii huhitajika kwa wagonjwa ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri.

Hospitali hizo ni Njombe, Sokoine Lindi, Singida, Kitete –Tabora, Simiyu, Rukwa, Ruvuma, Mbeya, Shinyanga, Geita na Dodoma.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Aprili 30, 2026 na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe alipokuwa akizungumza na Mwananchi kuhusu changamoto ya ukosefu wa huduma ya dialysis katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe.

“Tayari hili lilikuwa linashughulikiwa kwa kutambua umuhimu wa matibabu haya, mashine nane zimeshapelekwa Njombe na sasa taratibu zingine zinaendelea,” amesema Dk Magembe.

Awali, wagonjwa wa figo Njombe walilazimika kusafiri kwenda mikoa ya Mbeya au Dar es Salaam kupata huduma.

Hili liliongeza gharama za usafiri, malazi na hata kuhatarisha maisha kwa kuchelewa matibabu.

Akifafanua zaidi kuhusu kuanzisha matibabu hayo katika hospitali hiyo na maeneo mengine nchini, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema jumla ya hospitali 11 zitaanza kutoa huduma hiyo ifikapo Julai mosi mwaka huu, Njombe ikiwamo.

Amesema Njombe ni miongoni mwa hosptali zilizokuwa hazina huduma za dialysis, lakini tayari utaratibu umefanyika, akibainisha hatua zilizopo sasa hivi ni kuandaa namna huduma zitakavyoanza kutolewa Julai mwaka huu.

“Kwa sasa ni maandalizi ya chumba cha kutolea hizo huduma, watumishi kupata mafunzo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma na kuziweka sawa mashine,” amefafanua.

Dk Nyembea amesema hospitali za rufaa za mikoa ambazo ni za Serikali, zinazotoa huduma kwa sasa ni 16 kati ya 28 zilizopo nchini, na zile ambazo zinaandaa kuanza kutoa huduma kwa mwaka mpya wa fedha ni 11.

Dk Nyembea amesema baada ya kufungwa mashine hizo, itabaki Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songwe pekee, kuanza kutoa huduma hizo.

Alipoulizwa kuhusu mafunzo kwa watoa huduma amesema, “wataalamu huwa wanapatiwa mafunzo ya muda mfupi, wanakwenda kwenye hospitali zinazotoa hizo huduma.

Njombe watakwenda Hospitali ya Kanda ya Mbeya ambako pale tayari kuna madaktari bingwa bobezi wa hiyo huduma, watawafundisha kwa muda wa miezi mitatu kisha watakuwa wameiva kwa ajili ya kuja kutoa huduma.”

Amesema licha ya kuanza kutoa huduma, watatembelewa na daktari bingwa bobezi wa figo kila baada ya muda mfupi kwa ajili ya kuona wagonjwa ambao wanahitaji kuonwa na mtaalamu huyo.

Hatua hiyo inamechukuliwa wakati ambao takwimu zinaonesha wagonjwa wanaopata huduma ya kusafisha damu imeongezeka kutoka 1,017 mwaka 2019 hadi kufikia 3,342 mwaka 2026.

Miongoni mwa changamoto zinazowasibu wagonjwa wenye magonjwa sugu ya figo ni usafishaji damu, huduma ambayo mgonjwa hupatiwa mara tatu kwa wiki, ili aendelee kuishi wakati akisubiri upandikizaji wa figo.

Gharama za usafishaji figo zimeendelea kushuka mwaka hadi mwaka mpaka kufikia kiasi cha Sh150,000 kwa mzunguko mmoja, hivyo mgonjwa kuhitaji Sh450,000 kwa mzunguko wa wiki moja.

Ili kukabiliana na gharama kubwa ya huduma ya usafishaji wa damu kwa wenye ugonjwa sugu wa figo, mashine mpya aina ya SWS 6000 ziliingizwa nchini ambazo zilishusha gharama ya tiba hiyo kutoka Sh250,000 mpaka Sh150,000.

“Kwa mashine ambazo tunazitumia nchini ambazo zinauzwa na Bohari ya Dawa (MSD) bei yake ni Sh40 milioni,” amesema Dk Nyembea.

Kwa mujibu wa taarifa ya MSD, gharama za vitendanishi kwa kifurushi (Kit) ya kipindi kimoja cha dialisisi kwa mgonjwa imeshuka kutoka wastani wa Sh179,000 mpaka wastani wa Sh70,160 inayopatikana MSD.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya huduma za figo nchini zimeimarika, huku vituo vya kusafisha damu vikiongezeka hadi kufikia 73 vyenye mashine 749 zinazohudumia wagonjwa 3,342.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa wagonjwa 158 wamefanikiwa kupandikizwa figo nchini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaonya kuwa ugonjwa huo unaongezeka kwa kasi na unakadiriwa kuwa miongoni mwa magonjwa matano yatakayosababisha vifo vingi duniani ifikapo mwaka 2050 endapo hatua za kinga hazitachukuliwa.

WHO inaeleza kuwa mtu mmoja kati ya watano wenye shinikizo la damu huathiriwa na ugonjwa wa figo, huku watu wanne kati ya 10 wenye kisukari pia wakikumbwa na tatizo hilo.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wameonya kuwa mtindo wa maisha unaohusisha matumizi makubwa ya soda, vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) na vilevi, huku watu wakipunguza unywaji wa maji ya kutosha, inaongeza hatari ya kupata magonjwa ya figo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *