
Dar es Salaam. Makali ya ongezeko la nauli kwa usafiri wa daladala, mabasi ya mikoani na teksi mtandao yameanza kuuma leo Ijumaa, Mei Mosi 2026, hatua inayokuja baada ya kupanda kwa bei ya mafuta.
Kuanza kutumika kwa nauli hizo ni baada ya kukamilika kwa siku 14 tangu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) ilipozitangaza katika Gazeti la Serikali Aprili 17, 2026.
Kwa mujibu wa tangazo hilo la Latra, nauli za teksi mtandao zitakuwa Sh4,000 hadi Sh5,000, huku gharama ya kuanzia safari itakuwa kati ya Sh1,100 na Sh1,200. Aidha, nauli kwa kila kilometa ni kati ya Sh1,100 hadi Sh1,300 na kwa dakika ni kati ya Sh120 hadi Sh150.
Kwa upande wa nauli za mabasi ya mijini (daladala) zimeongezeka kwa Sh100 kwa kila safari, ambapo sasa kiwango cha chini kimefikia Sh700 kutoka Sh600 kwa umbali usiozidi kilometa 10.
Aidha, nauli za safari ndefu zimepanda kulingana na umbali, huku baadhi ya mikoa ikishuhudia ongezeko kubwa, ikiwemo Mwanza (Sh9,000), Morogoro (Sh2,000), Dodoma (Sh4,000) na Arusha (Sh5,000).
Mabadiliko hayo ya bei yanatokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta kulikosababishwa na mgogoro Mashariki ya Kati, unaohusisha mataifa ya Marekani, Israel na Iran. Mgogoro huo umesababisha kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz unaopitisha asilimia 20 ya mafuta yote duniani.
Akizungumza na Mwananchi Alhamisi, Aprili 29, 2026, Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Shifwanya Lema, amesema kwenye kikao walichokaa na mamlaka husika walikubaliana kiwango kitakachoongezeka ni Sh100 katika kila safari.
Amesema mabadiliko ya nauli yanayoshuhudiwa katika baadhi ya njia yametokana na tathmini ya gharama za uendeshaji, akisisitiza kuwa hatua hiyo imelenga kuendana na hali halisi ya kiuchumi na gharama ya mafuta.
“Tulifanya mazungumzo na mamlaka husika na makubaliano tutaongezewa Sh100 katika kila safari na Sh200 kwa wanafunzi, na hii ipo wazi,” amesema Lema.
Amesema walifanya mazungumzo ya pamoja ili kuangalia mwenendo wa gharama, ikiwa ni pamoja na kupanda au kushuka kwa baadhi ya mahitaji muhimu katika uendeshaji.
Amesema mabadiliko hayo yanatofautiana kulingana na eneo na hakuna sehemu imeongezeka zaidi ya hapo; hesabu za kilometa zisiwachanganye wananchi.
Katibu huyo amesema lengo si kuwaumiza abiria bali kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa bila kukwama.
“Hatujalenga kuwaongezea mzigo abiria, lakini pia tunahitaji kuhakikisha shughuli zinaendelea; hatuwezi kuendesha bila kuangalia gharama halisi,” amesema.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wanafunzi kutojazana vituoni kwa kusubiri gari moja wakati wa kazi ili kuondoa usumbufu na lawama kwa madereva na makondakta kwa kukataliwa.
“Niwaombe wanafunzi wasichague magari na wote kutaka kupanda gari moja. Nauli yao imebaki Sh200 kama ilivyokuwa awali, lakini wasitumie mwanya huo kujazana kwenye gari moja na kuwa chanzo cha lawama,” amesema.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John, amesema kinachotakiwa kwa abiria kuelewa ni kufanya hesabu ya kuzidisha kutokana na umbali wa safari.
“Hapo ni kuzidisha tu: kuchukua kiwango cha pesa kilichowekwa mara kilometa ya mtu anapokwenda. Mfano, wanaokwenda Mwanza imeongezeka Sh9,000 kwa magari ya kawaida, Dodoma Sh4,000, Morogoro Sh2,000 na Arusha Sh5,000,” amesema John.
Amesema kilichowekwa ni cha kawaida kulingana na hali halisi iliyopo kwa sasa, hivyo kila mmoja anapata nafuu kwa upande wake mfanyabiashara na abiria.
Dereva wa daladala ya Pugu Stesheni–Mwenge, Mahamoud Amri, amesema kwa sasa wanakwenda kubadilisha nauli kwenye milango kwa ajili ya kuanza kutumia rasmi nauli husika.
“Daladala leo na kesho tunaenda kuchora nauli mpya. Hata hivyo, bado tunafanya vitu kirafiki kwa sababu tukifika vituo kadhaa kabla ya kufika mwisho huwa tunashusha nauli,” amesema Amri.
Naye dereva wa teksi mtandao, Richard Kobelu, amesema wanachofuatilia kwa sasa ni kamisheni baada ya kubadilika kwa nauli, kwani mafuta yalishapanda lakini walibaki katika kiwango cha awali.
Tangazo la Bolt
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Aprili 29, 2026, na Kampuni ya huduma za teksi mtandao ya Bolt, imesema itaanza kutekeleza ongezeko la nauli la asilimia 22 kuanzia Mei Mosi 2026, kutokana na ongezeko la asilimia 33.4 la bei za mafuta nchini.
“Marekebisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa hatua za udhibiti zilizolenga kuimarisha uthabiti wa sekta ya usafiri wakati wa kupanda kwa gharama za uendeshaji.
“Mafuta yanaendelea kuwa miongoni mwa gharama kubwa kwa madereva, na muundo mpya wa nauli unakusudia kupunguza athari za shinikizo endelevu la bei za mafuta,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa dhamira ya Bolt ni kusawazisha unafuu wa nauli kwa abiria na mapato endelevu kwa madereva, huku ikiwahakikishia huduma zitaendelea kutolewa katika maeneo yote.
“Tunaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka husika ili kuimarisha mfumo thabiti na unaozingatia kanuni katika sekta ya usafiri wa mtandao wakati wa kipindi hiki cha mpito.
“Bolt inabaki na dhamira ya uwazi, usalama na uendelevu wa muda mrefu katika mfumo wa usafiri nchini Tanzania,” imeeleza.