
Rais wa Iran: Mzingiro wa kijeshi baharini ni tishio kwa amani ya dunia
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa jaribio lolote la kuweka vikwazo au mzingiro wa kijeshi katika njia za bahari linakiuka kanuni za kimataifa na linahatarisha maslahi ya mataifa ya eneo hilo pamoja na amani na uthabiti wa dunia, na hatimaye halitafanikiwa.
Katika ujumbe wake uliotolewa Alhamisi kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi, Pezeshkian amesema siku hii ni fursa muhimu ya kukumbusha tena ukweli wa kihistoria kwamba njia hii ya maji ni sehemu “isiyotenganishwa” na utambulisho wa Wairani, na pia ni alama ya mapambano ya taifa hili kubwa dhidi ya ukoloni wa zamani na wa kisasa.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika katika mazingira ambayo vita vya kulazimishwa vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu vimeonyesha tena umuhimu wa eneo hili kwa dunia, hususan Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Rais Pezeshkian amesema maadui wa Iran wamebadili mbinu za shinikizo kutoka kwenye sekta ya uchumi hadi kwenye juhudi za kuzuia au kudhibiti usafiri wa baharini na biashara kupitia njia za majini, kama njia mpya ya kulishinikiza taifa na serikali ya Iran.
Amesisitiza kwamba, “kama ambavyo tumekuwa tukitangaza mara kwa mara, uwepo na uingiliaji wa mataifa ya kigeni hautasaidia kuimarisha usalama wa eneo hili, bali utachochea mvutano na kuvuruga amani ya kudumu katika Ghuba ya Uajemi.”
Aidha alisema kwamba katika kipindi cha siku 40 cha mashambulizi ya Marekani na Israel, imebainika kuwa kambi za kijeshi za Marekani katika nchi za eneo hazikuweza kuhakikisha usalama wa nchi zinazozikaribisha, na badala yake ziliweka hatarini amani na usalama wao.
Rais Pezeshkian amesisitiza pia kwamba Iran, kama mlinzi wa usalama wa Ghuba ya Uajemi na Mlango wa Hormuz, inaendelea kushikamana na kanuni za uhuru wa urambazaji wa baharini na usalama wa majini, isipokuwa kwa nchi zinazochukuliwa kuwa na uhasama.
Pezeshkian Marekani na utawala wa Israel zinabeba dhima ya hali yoyote ya ukosefu wa usalama katika njia hiyo muhimu ya bahari.
Mwisho, amebainisha matumaini kwamba usalama na uthabiti wa kudumu vitarejea katika Ghuba ya Uajemi bila uwepo wa majeshi ya tawala za kigeni.