WACHEZAJI wa Simba wamevuna mamilioni kama zawadi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano, huku ushindi huo ukiwaumiza Yanga ambao wamekosa Sh300 milioni ambazo waliahidiwa na mfadhili wa klabu hiyo Gharibu Said ‘GSM’.
Yanga Aprili 29, 2026 ilipoteza mchezo wa fainali wa Kombe la Muungano kwa kulala bao 1-0 dhidi Simba katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar na sasa inatarajiwa kujiuliza kwenye Dabi ya Ligi Kuu Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni jijini Dar es Salaam.
Simba ilikabidhiwa Fedha hizo jana mara baada ya kikosi hicho kuwasili jijini Dar es Salaam kikitokea Zanzibar walikokuwa wakishiriki michuano hiyo na kufanikiwa kuibuka mabingwa kwa kishindo, ukiwa ni ubingwa wao wa pili tangu mashindano hayo yaliporejea.
Mbali na fedha hizo, Simba imeandika rekodi ya kipekee kwa kuendeleza ubora wao katika Kombe la Muungano, ikiwa ni miongoni mwa timu zenye mafanikio makubwa zaidi kwenye michuano hiyo baada ya kutwaa ubingwa mara saba.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zililiambia Mwanaspoti kuwa Simba jumla wamepewa Sh500 milioni, zawadi hiyo ni sehemu ya motisha iliyowekwa na uongozi kwa ajili ya kuhakikisha wachezaji wanapambana na kuleta matokeo chanya, jambo ambalo limezaa matunda.
“Ushindi huo umeendelea kuonesha uimara wa Simba, huku wachezaji wakionekana kuwa na morali ya hali ya juu kutokana na kuthaminiwa kwa juhudi zao, wakijiwekea rekodi ya kutwaa ubingwa huo mara kadhaa tofauti na baadhi ya wapinzani wao. ‘’Motisha waliayoahidiwa wamepewa kabla ya mchezo mwingine wa dabi Jumapili ili kuwaongezea morali ya kuhakikisha kuwa wanapata ushindi kwenye mechi hiyo muhimu ya ligi.”
YANGA KILIO
Wakati Simba wakifurahia mafanikio hayo na rekodi walizoweka, hali imekuwa tofauti kwa watani wao wa jadi Yanga, ambao wamejikuta wakipoteza donge nono la fedha.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga zilisema kuwa, wachezaji wa Yanga wamekosa kiasi cha Sh300 milioni, fedha ambazo zilikuwa zimeahidiwa na mfadhili wao GSM endapo wangefanikiwa kutetea ubingwa wa Kombe la Muungano.
“Kupoteza ubingwa huo kumewagharimu si tu heshima ya taji, bali pia mapato hayo makubwa ambayo yangekuwa kichocheo kwao kumaliza msimu kwa nguvu zaidi.
“Haya matokeo yanaongeza presha kwa Yanga, huku mashabiki wakitarajia kuona mabadiliko na mrejesho wa haraka kutoka kwa timu yao katika mashindano yajayo,” ilisema taarifa.
Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa kileleni na pointi 47 tano mbele ya Simba iliyopo nafasi ya pili huku timu zote zikicheza michezo 19.