Marekani. Mwanamuziki maarufu wa Pop kutokea Marekani, Ariana Grande (32), ametangaza rasmi ujio wa albamu yake mpya na ya nane inayotarajiwa kuachiwa hapo Julai 31 mwaka huu.
Albamu hiyo iliyopewa jina la Petal, tangazo la ujio wake limetolewa na Ariana mwenyewe kupitia mitandao yake ya kijamii, ambapo pia alionyesha na cover lake.
Cover hilo lina picha yenye rangi nyeusi na nyeupe inayomwonyesha Ariana akiwa ameachia nywele zake huku akitabasamu.
Katika maelezo yake, msanii huyo amesema albamu hiyo imejaa muziki uliobeba hisia huku ikielezea safari yake ya kukua na kuvuka changamoto ngumu za kimaisha.
Albamu hiyo imeandikwa na kutayarishwa kwa kushirikiana na mtayarishaji wake wa muda mrefu, Ilya, na inatarajiwa kuwa na jumla ya nyimbo 12.
Albamu hii inakuja kufuatia mafanikio ya albamu yake iliyopita, Eternal Sunshine (2024) ambayo ilifanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye chati ya Billboard 200.
Vilevile albamu hiyo ilitoa nyimbo maarufu kama ‘Yes, And?’ na ‘We Can’t Be Friends (Wait for Your Love)’ zilizofika namba moja kwenye Billboard Hot 100.
Kwa sasa Ariana anajiandaa kuanza ziara yake ya kimuziki itakayoanza Juni 8 na kumalizika Septemba mosi, hii ni ziara ambayo ndani yake kuna ratiba ya kufanya show 10 jijini London, Uingereza.
Awali msanii huyo ambaye pia ni mwigizaji wa filamu, alikuwa amedokeza kuwa hataachia wimbo mpya kwa kipindi hiki ili kujikita kwenye uigizaji.
Hata hivyo, wiki chache zilizopita alianza kutoa ratiba yake ya kurejea studio, jambo ambalo sasa limethibitishwa rasmi kupitia tangazo la albamu ya Petal.
Ikumbukwe albamu sita za Ariana zimefika nafasi ya kwanza kwenye chati ya Billboard 200, huku nyimbo tisa zikishika nafasi ya kwanza kwenye Billboard Hot 100.
Akiwa tayari ameshinda tuzo tatu za Grammy, na tuzo 13 za MTV VMAs, Ariana anatambulika kama mmoja wa wasanii waliouza zaidi duniani ambapo mauzo yake yanakadiriwa kufikia rekodi milioni 90.
Staa huyu ni mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa duniani akishika nafasi ya sita kwa kuwa na wafuasi (followers) wengi katika mtandao wa Instagram ambapo watu milioni 371 wanamfuatilia.
Majarida kama Rolling Stone na Billboard yamemtaja Ariana kuwa mmoja wa wasanii wakubwa zaidi katika historia, huku Time ikimjumuisha kwenye orodha ya watu 100 wenye waliokuwa na ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa mwaka 2016, na 2019.