Dar es Salaam. Ikiwa ni mwezi mmoja tangu Bien wa Kenya kuachia wimbo wake, Finale (2026) akishirikiana na Alikiba, mapokezi yake ndani ya muda huo yanatoa picha ya kile kinachoenda kutokea katika tasnia ya muziki nchini humo.
Bien aliyevuma kwa mara ya kwanza kupitia kundi la Sauti Sol, huu ndio wimbo wake kwanza kupata mapokezi makubwa zaidi tena ndani ya muda mfupi tangu ameanza kufanya kazi peke yake (solo) mwaka 2023.
Ndani ya mwezi mmoja tu, video ya wimbo ‘Finale’ imetazamwa (views) YouTube zaidi ya mara milioni 20, na kuandika rekodi kama video ya kwanza ya muziki Kenya kufanya hivyo, hatua ambayo ni heshima kubwa kwa Bien.
“Namshukuru Mungu kwa baraka zisizo na kikomo anazoendelea kutujalia. Kwa mashabiki ambao ni sawa na upepo chini ya mabawa zetu, asanteni sana kwa ‘views’ milioni 20,” alieleza Bien kupitia mitandao yake ya kijamii.
Je, hatua hii ina maana gani kwa Bien na tasnia ya muziki Kenya kwa ujumla? Hatua hii inamuweka Bien katika nafasi ya kuja kuwa msanii mwenye wimbo uliotazamwa (most viewed) zaidi YouTube nchini huko kwa muda wote!.
Hatua hiyo kubwa itafikiwa endepo tu ‘Finale’ itaendelea kufanya vizuri kwa kiwango hiki, na hivyo tutarajie rekodi hiyo kuwekwa ndani ya kipindi cha takribani miezi miwili hadi mitatu kwa kuanzia sasa.
Hadi sasa video inayoshika namba moja kwa kufanya vizuri YouTube Kenya, ni ya wimbo wa Willy Paul, I Do (2017) ambayo imetazamwa mara milioni 46 ikiwa ni zaidi ya miaka minane tangu kuachiwa kwake.
Hata hivyo, kumekuwa na kutofautiana mtazamo kuhusu rekodi hiyo kwani wapo wanaoutaja wimbo wa Willy Paul akimshirikisha Rayvanny, Mmmh (2019) ambao video yake imeshatazamwa mara milioni 49.
Licha ya wimbo huu kuwa wa msanii wa Kenya lakini chati mbalimbali nchini humo zinaonyesha kutoutambua na hii kwa sababu video yake iliwekwa katika chaneli ya YouTube ya Rayvanny, na si Willy Paul ambaye ndiye mmiliki wake.
Yote kwa yote, ukitazama namba za video hizo mbili (I Do – milioni 46, & Mmmh – milioni 49), utabaini kuwa ‘Finale’ imetumia mwezi mmoja kufikia takribani nusu ya namba hizo, na ndio sababu tunasema kati ya miezi miwili hadi mitatu ijayo inaweza kuwa namba moja.
Hatua hiyo itakuwa na maana kubwa katika Bongofleva kwani itakuwa ni rasmi video za muziki Kenya vilizofanya vizuri YouTube, tatu wameshirikishwa wasanii wa Bongofleva nyingine ni ya wimbo wa Otile Brown, One Call (2023) akiwa na Ruby ambayo imetazamwa mara milioni 39.
Wakati ‘Finale’ ya Bien na Alikiba ikiandika rekodi ya kuwa video ya kwanza Kenya kutazamwa YouTube mara 20 kwa mwezi mmoja, rekodi kama hiyo kwa Tanzania inashikiliwa na Diamond Platnumz kupitia wimbo wake, Waah! (2020) akimshirikisha Koffi Olomide kutokea DR Congo.
Video hiyo ya Diamond na Koffi ilitazamwa mara milioni 20 YouTube ndani ya wiki tatu tu!, na hadi sasa hakuna video ya nyingine ya Diamond na kutokea Tanzania kwa ujumla iliyoweza kuweka rekodi za kibabe kama hiyo.
Ikiwa tayari imetazamwa (views) mara milioni 194.8, rekodi zake zilikuwa kama ifuatavyo ‘views’ milioni 1 ndani saa nane, milioni 4 ndani ya saa 48, milioni 10 ndani ya wiki moja, milioni 20 kwa wiki tatu, milioni 30 kwa mwezi mmoja, milioni 40 kwa miezi miwili, na milioni 50 kwa miezi mitatu!.
Hivyo basi, ikiwa ‘Finale’ ya Bien na Alikiba itafikisha ‘views’ milioni 50 kwa miezi mitatu kama nilivyotangulia kueleza, si kwamba tu itaweza kuwa video namba moja Kenya kwa kutazamwa zaidi YouTube, bali itaifikia rekodi hiyo ya kolabo ya Diamond na Koffi Olomide.
Ikumbukwe ‘Finale’ ni wimbo unaozungumzia starehe ambapo Alikiba na Bien wanafurahia pamoja na wale wanaowapenda, ila kubwa zaidi unazungumzia kufika mwisho wa safari ya kusaka mapenzi ya kweli.
Mhusika mkuu wa wimbo huu ni mwanaume ambaye amepitia mahusiano mengi yenye changamoto lukuki lakini sasa anaamini kuwa amempata yule anayemfaa katika maisha yake.
Neno “Finale” linamaanisha mwisho wa kutafuta na mwanzo wa uhusiano wa dhati wenye kujitoa kwa asilimia 100 kwa pande zote mbili.
Ukiwa umetayarishwa na Abbah na Hendricks Sam, wimbo huu umechanganya ladha ya Afropop na Bongofleva, huku ukibebwa zaidi na sauti nzuri na uwasilishaji wenye kuvutia, jambo linaloufanya kuwa moja ya kolabo bora Afrika Mashariki.